Rais Dkt. John Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Steven Kebwe kufikisha salamu zake za pole kwa familia na wote walioguswa na vifo vya watu zaidi ya 60 na majeruhi takribani 70 walioungua kwa moto baada ya lori lililokuwa na shehena ya mafuta kupata ajali na kisha kulipuka moto Mjini Morogoro.
Rais Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya ajali hiyo iliyotokea leo tarehe 10 Agosti, 2019 majira ya saa 2 asubuhi ambapo lori hilo lililokuwa linatoka Dar es Salaam limepinduka jirani na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu baada ya dereva wa lori kumkwepa mwendesha pikipiki na kisha mafuta yaliyokuwa yakimwagika kushika moto na kuunguza watu waliokuwa wanaya chota.
Ameziagiza Wizara zote zinazohusika kushughulikia ajali hii na ametaka Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwakushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili kuhakikisha majeruhi wote wanapatiwa matibabu ili kuokoa Maisha yao.
Rais Magufuli ametoa pole kwa familia, ndugu, marafiki na wote waliopoteza jamaa zao katika ajali hii na pia amewaombea majeruhi wapone haraka.
“Nimeumia sana kusikiai dadi kubwa ya Watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali hii, natoa pole kwa wote walioguswa na vifo hivi hasa familia za Marehemu wote, nawaombea Marehemu wapumzike mahali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka” amesema.
Aidha, Rais Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na vitendo vya watu kuvamia magari yanayopata ajali kwa lengo la kujipatia bidhaa mbalimbali zilizobebwa na magari hayo na ametaka vitendo hivyo vikome.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇