Moto wa hasira umezuka kila pembe ya Marekani baada ya kusambaa kwenye mitandao ya kijamii picha inayowaonyesha askari polisi wawili waliopanda farasi wakimpeleka kituoni katika mji wa Galveston jimboni Texas raia mweusi, huku wakiwa wamemfunga kamba, kitendo ambacho kimekumbusha historia ndefu ya ukatili, utumwa na ubaguzi wa rangi dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika, katika enzi za utenganishaji jamii za watu wa nchi hiyo.
Raia huyo mweusi Donald Neely alikamatwa na askari hao siku ya Jumamosi iliyopita kwa kosa la kuvamia milki ya watu.
Kufuatia kitendo hicho, mkuu wa polisi wa mji wa Galveston Vernon Hale ametoa taarifa ya kuomba radhi; hata hivyo taarifa yake hiyo imekabiliwa na ukosoaji mkubwa zaidi kwa kutajwa kuwa ni hatua "dhaifu".
Hale amesema, ilipasa Neely apelekwe kituoni kwa gari ya polisi badala ya kuchukuliwa na askari wapanda farasi.
Hata hivyo kauli hiyo imekosolewa na wanaharakati na makundi ya kutetea haki wakisisitiza kuwa ni "dhaifu" na "haitoshi".
Clayborne Carson wa chuo kikuu cha Stanford amesema, mtu yeyote hata mwenye uelewa mdogo tu wa historia ya Marekani, anaelewa maana ya kumuona mtu mweusi akiendeshwa kwa miguu kama alivyofanyiwa Donald Neely, na kuongeza kwamba, kitendo hicho kinatoa mtikisiko mkubwa wa taswira mbaya zaidi ya ubaguzi wa rangi wa enzi za utumwa.
Wanaharakati wengine wametoa wito wa kutaka askari hao wawili wa polisi ya Marekani wapewe adhabu au kufukuzwa kazi kwa kile walichokiita kuwa ni kumdhalilisha Neely.
Tukio hili limejiri katika hali ambayo, chunguzi mbali mbali za maoni zilizofanywa zinaonyesha kuwa, Wamarekani wengi wanaamini kwamba ubaguzi wa rangi lingali ni tatizo kubwa na muhimu katika jamii yao, na kwamba hali hiyo imeshadidi na kupamba moto tangu Donald Trump ashike hatamu za urais wa nchi hiyo.../
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇