Polisi nchini Zambia imemtia mbaroni mkuu wa chama kidogo cha upinzani nchini humo kwa madai ya kumkashifu Rais wa nchi hiyo Egdar Lungu na kumtaja kuwa ni mbwa.
Chishimba Kambwili mkuu wa chama cha National Democratic Congress (NDC) ametetea matamshi yake na kuwaambia waandishi habari kwamba, maneno hayo aliyoyatoa kwa njia ya video yametafsiriwa vibaya. Kambwili na wanasiasa wengine wa upinzani Zambia wanamtuhumu Rais Lungu kuwa anatekeleza siasa za kuwakandamiza; tuhuma ambazo zimekuwa zikikanushwa na serikali ambayo inasema kuwa inalinda uhuru wa kujieleza.
Kiongozi huyo wa chama kidogo cha upinzani nchini Zambia alikamatwa jana siku mbili baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kufuta usajili wa chama chake cha NDC akisema kuwa chama hicho kimekiuka katiba yake. Kambwili amesema atahoji mahakamani uamuzi huo wa kufutiwa usajili chama chake.
Chama cha Kambwili mwaka 2016 kilijitenga na chama cha Edgar Lungu cha Patriotic Front na kisha kikashinda kiti chake cha kwanza bungeni katika uchaguzi wa mwezi Aprili katika eneo bunge lililokuwa likishikiliwa na chama tawala.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇