Kikao cha siku mbili cha viongozi wa kundi la G7 linaloundwa na nchi saba kubwa za viwanda, yaani Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Japan, Italia na Canada kinaanza Jumamosi ya leo ya tarehe 24 Agosti nchini Ufaransa, huku kukishuhudiwa madukuduku na tofauti zilizojitokeza kati ya Marekani na wanachama wengine wa kundi hilo.
Nchi zinazounda kundi la G7 zinahodhi zaidi ya nusu ya uchumi wote wa dunia. Viongozi wa nchi wanachama wa kundi hilo huwa na kikao cha pamoja mara moja kila mwaka.
Tangu Donald Trump alipoingia madarakani Januari 2017 na kushika hatamu za urais wa Marekani, uhusiano wa nchi zilizoko kwenye pande mbili za Bahari ya Atlantiki umekuwa wa vuta nikuvute. Kwa kutumia siasa za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja, rais wa Marekani amekuwa akijaribu kuwatwisha mitazamo na matakwa yake mbali mbali washirika na waitifaki wa Washington. Suala hilo limedhihirika pia katika kundi la G7. Moja ya tofauti zilizojitokeza kabla ya kufanyika kikao cha viongozi wa kundi hilo nchini Ufaransa ni takwa la Trump la kujiunga tena Russia katika G7. Russia iliwekwa kando ya vikao vya madola manane makubwa ya viwanda mwaka 2014 kwa sababu ya kile kilichodaiwa na nchi za Magharibi kuwa ni kuhusika na kuingilia kwake katika mgogoro wa Ukraine; na tangu wakati huo hadi sasa kikao hicho kinafanyika katika muundo wa kundi la G7. Hata hivyo Trump anashikilia Moscow ialikwe tena kuhudhuria kikao cha kundi hilo. Siku chache zilizopita, rais huyo wa Marekani alisema, anaunga mkono Russia kujiunga tena na kundi la G7 na kubadilika muundo wake kuwa wa G8. Hii si mara ya kwanza kwa Trump kuunga mkono wazo la Russia kujiunga tena na kundi la nchi saba kubwa za viwanda. Mwaka jana pia wakati wa kukaribia kufanyika kikao cha G7 nchini Canada, rais huyo wa Marekani alilipigia upatu wazo hilo. Kwa mujibu wa Trump: Endapo Russia itarudi kwenye kundi la G7, mijadala juu ya masuala mengi itakuwa myepesi zaidi.
Pamoja na hayo, takwa hilo la rais wa Marekani limepingwa na wanachama wa Ulaya katika kundi la G7. Nchi hizo, na hasa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zimelifungamanisha suala hilo na kubadilika siasa za Russia kuhusiana na Ukraine. Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anasema, suala hilo linafungamana moja kwa moja na utekelezwaji wa makubaliano ya Minsk kuhusu Ukraine. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, ambaye siku chache nyuma alimlaki Rais Vladimir Putin wa Russia na kufanya mazungumzo naye mjini Paris, alisisitiza katika mazungumzo yao kwamba, bila kutatuliwa mgogoro wa Ukraine, Russia haitaruhusiwa kurejea kwenye kundi la G8, ambalo sasa limekuwa G7 baada ya kuondolewa Moscow. Hata hivyo upinzani mkubwa zaidi dhidi ya wazo la kurejea tena Russia katika G7 umeonyeshwa na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, ambaye kutokana na madai ya London ya kuhusika Russia katika kumpa sumu jasusi wa zamani wa nchi hiyo Sergei Skripal na binti yake Yulia nchini Uingereza, na vile vile kwa sababu ya Moscow kuendeleza msimamo ilionao kuhusiana na Ukraine, yeye pia anapinga wazo la kuiruhusu Moscow ijiunge tena na G7. Kuhusu pendekezo hilo la Trump, Rais Putin wa Russia amesema, nchi yake inaamini kwamba, kuwa na uhusiano wa aina yoyote na kundi la G7 kuna faida; na si baidi kwa Russia kurejea kwenye kundi hilo la madola makubwa saba ya viwanda.
Suala jengine ambalo tokea sasa inaonekana kwamba litazusha mvutano na kutawala katika majadiliano ya viongozi wa G7 ni ung’ang’anizi wa Trump wa kutaka wanachama wengine wa kundi hilo wafuate sera za Washington hususan za uchumi. Inategemewa kuwa atakapokutana na viongozi wenzake wa G7 katika kikao cha Ufaransa, rais huyo wa Marekani ataitumia fursa hiyo kusifu sera za kiuchumi za serikali yake na kuwashawishi waitifaki hao wa Washington wafuate kigezo cha nchi hiyo katika kutatua matatizo ya uchumi wa dunia. Trump anatazamiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Japan, India na Canada. Shirika la habari la Reuters limesema, mazungumzo ya rais wa Marekani na viongozi wa nchi hizo yatakuwa “tata” na magumu kwa sababu sera za kibiashara za Trump zimesababisha tofauti na hitilafu kubwa kati ya serikali ya Marekani na za nchi zingine za kundi la G7.
Kwa kutilia maanani siasa za uchukuaji maamuzi ya upande mmoja zinazotekelezwa na Trump na msimamo wake wa kutaka kuwabebesha wanachama wengine wa G7 mawazo na matakwa yake, majadiliano makali yanatazamiwa kutawala kikao cha Ufaransa. Kikao kilichopita cha Juni 2018 kilichofanyika nchini Canada, nacho pia kilishuhudia mabishano ambayo hayajawahi kushuhudiwa kati ya Trump akiwa upande mmoja, na viongozi wa Ulaya na Waziri Mkuu wa Canada katika upande mwingine; kiasi cha kuwafanya wachambuzi wa siasa waamue badala ya G7, kubuni istilahi mpya ya 6+1 kwa ajili ya kundi hilo la madola makubwa saba ya viwanda duniani…/
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇