LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 20, 2019

BALOZI SEIF AKEMEA MAKUNDI NDANI YA CCM

Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga ambaye ni Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, ameanza ziara ya siku tano mkoani Shinyanga, kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambapo pamoja na mengine  amekemea kuwepo na makundi ndani ya chama hicho.

Ziara ya Makamu huyo wa pili Zanzibar imeanza wilayani Kahama kwa kutembelea Jimbo la Msalala, na kukagua utekelezeaji wa ilani ya uchaguzi ya  CCM katika jimbo hilo, ambapo kesho atakuwa jimbo la Ushetu na Kahama Mji.

Akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Buganzo kata ya Ntobo halmashauri ya Msalala wilayani Kahama Mkoani Shinyanga, amekemea kuwepo na makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi CCM hasa kuelekea kwenye kipindi cha uchaguzi na kutaka kusiwepo na makundi hayo.

Amesema kuwepo kwa makundi ndani ya CCM, kuelekea kwenye kipindi hiki cha uchaguzi ni hatari, ambapo kutawagawa na kuwafanya kushindwa kupata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi na kuwapa nafasi wapinzani.

“Napenda kuwaambia wana CCM kwenye uchaguzi huu wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu ujao ushindi ni lazima, hivyo naomba kusiwepo na makundi ya aina yoyote ndani ya chama, pamoja na kutoweka wagombea wasio na sifa, bali pitisheni watu wanaokubalika kwa wananchi na waleta maendeleo,” amesema Balozi Iddi.

“Pia makatibu wa CCM ambao mna tabia ya kupitisha wagombea wenu wasio na sifa kwa sababu ya kufahamiana,naomba tabia hiyo muiache, kwani katika Serikali hii ya awamu ya tano tunataka washinde wagombea ambao wana sifa, waaminifu na wenye kuwatumikia wananchi kuwaletea maendeleo,” ameongeza Balozi Iddi.

Aidha amesema ili ushindi huo uweze kupatikana ni lazima watu wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura, pamoja na kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi, na kuchagua wagombea wa CCM, ambao ndiyo wenye kupigania maslahi ya wananchi.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages