Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa, kwa sasa serikali ya Washington haina mpango wa kuiwekea vikwazo Uturuki.
Trump ameyasema hayo kufuatia mzozo ulioshtadi kati ya nchi yake na Uturuki na kuongeza kuwa, kwa sasa hana mpango wa kuiwekea vikwazo nchi hiyo.
Hayo yanajiri ambapo Ikulu ya Marekani White House siku ya Alkhamisi ilitangaza kuwa, kwa kuzingatia hatua ya Uturuki ya kununua mfumo wa makombora wa S-400 kutoka Russia, ni suala lisilowezekana kuiuzia tena serikali ya Ankara, ndege za kivita aina ya F-35.
Aidha serikali ya Uturuki pia imetoa kauli kufuatia msimamo huo wa Washington ambapo İbrahim Kalın, Msemaji wa Rais Recep Tayyip Erdoğan amenukuliwa akisema kuwa, Ankara haijafurahishwa na hatua ya Washington ya kuiondoa nchi hiyo kwenye orodha ya pamoja ya kuunda ndege za kivita za F- 35.
Kabla ya hapo yaani tarehe 16 Julai mwaka huu, Rais Donald Trump wa Marekani alisema kuwa, hatua ya Uturuki ya kununua ngao ya makombora ya S -400 ya Russia, imeifanya Washington kufuta mpango wa kuiuzia nchi hiyo ndege zake za kivita za F 35.
Mkataba wa mauziano ya ngao ya makombora ya S-400 wa kiasi cha dola bilioni 2.5 kati ya Russia na Uturuki, ulitiwa saini Disemba 2017.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇