Kamanda wa operesheni maalumu za upelelezi wa jeshi la Israel amelazimika kujiuzulu kutokana na kushindwa operesheni ya Khan Yunis Novemba 2018 na kushindwa jaribio la kutaka kumuua mmoja wa makamanda wa ngazi za juu wa Brigedi ya Izzuddin Qassam, tawi la kijehi la harakati ya Hamas.
Mbali na mtikisiko na kuyumbayumba kisiasa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel, utawala huo haramu pia unasumbuliwa na kuyumbayumba katika upande wa masuala ya kiusalama. Sababu ya hali hii ni vita vya Novemba 2018 dhidi ya Ukanda wa Gaza. Wakati huo yaani tarehe 11 Novemba mwaka 2018, kundi la makomando wa utawala wa Kizayuni wa Israel lilishambulia eneo la mashariki mwa Khan Yunis. Lengo kuu la mashambulizi hayo lilikuwa kumuua kigaidi kamanda mmoja wa ngazi za juu wa Brigedi ya Izzuddin Qassam lakini matokeo ya vita hivyo yalikuwa kinyume kabisa na matarajio na yalizua mtetemeko na mtikisiko wa kisiasa na kiusalama ndani ya serikali ya Israel.
Makundi ya mapambano ya Palestina yalijubu mashambulizi hayo ya kikosi maalumu cha makomando wa Israel kwa "Operesheni ya Ncha ya Upanga". Mapigano makali yalitokea baina ya wanamapambano wa Kipalestina na askari wa utawala wa Kizayuni na askari kadhaa wa utawala huo wakaangamizwa. Makundi ya wanamapambano wa Palestina walivurumisha makombora na maroketi zaidi ya 500 dhidi ya vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina. Hali hii iliulazimisha utawala huo kukubali usitishaji wa vita baada ya siku nne tu za uvamizi huo, hatua ambayo ilitambuliwa na idadi kubwa ya wanasiasa na maafisa wa jeshi la Israel kuwa ni sawa na kukubali kushindwa mbele ya makundi ya mapambano ya Palestina.
Miongoni mwa athari muhimu za kisiasa za kushindwa huku ni kusambaratika baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu. Aliyekuwa waziri wa vita wa Israel, Avigdor Lieberman ambaye alitambua hatua ya kukubali kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza kuwa ni sawa na kushindwa mkabala wa wanapambano wa Kipalestina aliamua kuachia ngazi na kujiuzulu akilalamikia hatua hiyo.
Kujiuzulu huko kuliandamana na kusambaratika baraza la mawaziri la serikali ya mseto ya Netanyahu na kumlazimisha Waziri huyo Mkuu wa Israel kuitisha uchaguzi wa bunge mapema na kabla ya wakati wake. Uchaguzi huo ulifanyika Aprili mwaka huu. Hata hivyo Netanyahu aliyepewa jukumu la kuunda baraza jipya la mawaziri, alishindwa kuunda serikali mpya katika kipindi cha siku 42 kilichoainishwa kisheria na kwa msingi huo bunge hilo limevunjwa na umechukuliwa uamuzi wa kufanyika uchaguzi mwingine wa bunge mwezi Septemba mwaka huu. Mtetemeko na mkwamo huu wa kisaisa kwa hakika ni matokeo ya kushindwa jeshi la Israel katika operesheni ya Khan Yunis.
Athari nyingine mbaya ya kushindwa operesheni hiyo ni kujiuzulu kwa kamanda wa operesheni maalumu ya upelelezi wa kijeshi wa jeshi la Israel. Kujizulu huko kunapewa umuhimu mkubwa kwa kuzingatia kuwa, huyo aliyeng'atuka ni kamanda wa moja kati ya taasisi na nguzo muhimu za jeshi la utawala huo wa Kizayuni. Nafasi hiyo inapewa umuhimu mkubwa kiasi kwamba, kiongozi wake huonekana kwa nadra sana katika picha za vyombo vya habari. Nukta nyingine ni kuwa kamanda huyo wa Israel alijiuzulu nafasi hiyo yapata miezi miwili baada ya kushindwa operesheni ya Khan Yunis, suala linaloonesha uzito wa kushindwa kwa operesheni hiyo iliyowasomba waziri wa vita na kamanda wa taasisi muhimu ya jeshi.
Katika uwanja huo Hazim Qasim msemaji wa Harakati ya Mapambanbo ya Kiislamu ya Palestina Hamas amesema kwamba: Kujiuzulu kwa kamanda huyo wa jeshi la Israel kutokana na kipigo na kushindwa kwa operesheni ya Khan Yunis ni kielelezo cha pigo na dharuba kubwa iliyoupata utawala huo."
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇