Rais Dkt. John Magufuli ameitaka menejimenti na wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) kubadilika kwa kufanya kazi kwa tija wakati Serikali ya Tanzania na Zambia zikifanya juhudi za kuimarisha miundominu ikiwemo kununua injini na mabehewa mapya ya treni.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo leo wakati akizungumza na wafanyakazi wa TAZARA akiwa safarini kwa treni kutoka Dar es Salaam hadi Kisaki Mkoani Morogoro na baadaye kuelekea Rufiji ambako kesho atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za uwekaji jiwe la msingi katika mradi za kuzalisha umeme wa mto Rufiji.
Akizungumza na wafanyakazi wa TAZARA katika Stesheni ya Fuga, Rais Magufuli ameelezea kutofurahisha na taarifa za TAZARA kufanya kazi kwa kiwango cha chini ambapo kwa sasa inasafirisha tani 250,000 za mzigo kwa mwaka ikilinganishwa na uwezo wake wa tani 5,000,000 na imebakiwa na injini 5 zinazoendesha mabehewa 100 tu, ikilinganishwa na mahitaji ya injini 15 na mabehewa 700.
Rais Magufuli amesema kwa sehemu kubwa matatizo ya TAZARA yamesababishwa na menejimenti na wafanyakazi wa TAZARA ambao wamekuwa wakiiendesha tangu mwaka 1975 walipokabidhiwa baada ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Zambia kwa kushirikiana na China kuwekeza Dola za Marekani Milioni 500 (sawa na shilingi Trilioni 1 na Bilioni 140) na baadaye thamani yake kupanda hadi kufikia zaidi ya shilingi Trilioni 4.
“Nyinyi wafanyakazi wa TAZARA ndio mlioifikisha TAZARA hapa ilipofika, Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Mzee Keneth Kaunda wa Zambia waliwekeza kwenye mradi huu kwa kutambua umuhimu mkubwa wa reli hii, lakini nyinyi wafanyakazi mmepukutisha mpaka tumefika hapa, kuna mabehewa na injini hazifanyi kazi, matengenezo hayafanyiki, ni aibu uwekezaji wa TAZARA upotee bure namna hii,nataka mbadilike” amesisitiza Rais Magufuli.
Hata hivyo Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha TAZARA inaimarishwa na hivyo ameagiza mapendekezo ya mabadiliko ya sheria yatakayoruhusu kila nchi kuwekeza yaharakishwe ili uwekezaji huo utakaohusisha ununuzi wa injini nyingine na mabehewa ya mizigo na abiria ufanyike.
Akiwa katika safari hiyo, Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amesimama na kuzungumza na wananchi wa Gwata Wilayani Kisarawe ambapo amewaahidi kuwa Serikali itafanyia kazi maombi yao ya kutengenezewa barabara ya kutoka Gwata hadi Nzenga yenye urefu wa kilometa 32, kupatiwa umeme, kujengewa zahanati na ametoa mchango wa shilingi Milioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vya shule ya msingi Gwata.
Halikadhalika, Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Kisaki Mkoani Morogoro ambapo ameahidi kuwa Serikali itatoa shilingi Milioni 400 kwa ajili ya kuanza mara moja ujenzi wa Kituo cha Afya Kisaki na ameagiza uwanja wa kujenga kituo hicho upatikane ndani ya siku 7 kuanzia leo.
Pia ameendesha harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa Kituo cha Polisi Kisaki na kufanikisha kupatikana jumla ya shilingi Milioni 39.1 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho ambacho Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro ameahidi kukikamilisha ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.
Kuhusu malalamiko wa wakulima kudai wafugaji wamekuwa wakilisha mifugo kwenye mashamba yao, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe kuhakikisha migogoro hiyo inakoma, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wafugaji wanaolisha mazao kwenye mashamba ya wakulima wanakamatwa na wanachukuliwa hatua kali.
“Haiwezekani migogoro hii ya wakulima iendelee wakati viongozi mpo, mnafanya nini nahii migogoro haijaanza leo” ameeleza Rais Magufuli.
Ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha vijiji 2 vya Kata ya Kisaki ambavyo havina umeme vinapatiwa umeme haraka.
Aidha, amewataka wananchi wa Kisaki kuchangamkia fursa za mradi wa kuzalisha umeme wa mto Rufiji kwa kuzalisha mazao mengi na kujipatia ajira wakati wa ujenzi.

No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇