Jeshi la polisi nchini Tanzania limewapiga kalamu nyekundu askari wake 54 kuanzia Januari hadi mwezi Juni mwaka huu kutokana na kwenda kinyume na maadili ya kazi yao ikiwamo kufanya vitendo vya uhalifu na kushirikiana na wahalifu.
Hayo yamesemwa na Inspekta Jenerali wa Polisi nchini humo Tanzania (IGP), Simon Sirro ambaye amefafanua kuwa, hatua hiyo ni katika kujenga nidhamu na kuhakikisha uzalendo unachukua nafasi yake ndani ya jeshi hilo. Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa polisi Tanzania, kati ya askari hao wamo maafisa, wakaguzi na askari wa kawaida na kwamba walikumbwa na fagio hilo baada ya kukutwa na hatia za makosa mbalimbali. Sirro ambaye ameyasema hayo katika sherehe za uzinduzi wa nyumba za makazi za askari wa jeshi la polisi eneo la Magogo mkoani Geita amesema: “Wachache wanaokengeuka tunawachulia hatua, wajibu wetu ni kutenda haki na tunaendelea kuchukua hatua kwa wale wasio wazalendo, wasiotenda haki wanaoshirikiana na wahalifu kutorosha mali zetu.
Kama hawafuati mstari basi ni bora warudi uraiani waone maisha ya huko jinsi yalivyo.” Amesema IGP Sirro. Kwa upande wake Rais John Pombe Magufuli wa nchi hiyo wa Tanzania amempongeza IGP Sirro kwa hatua hizo za kinidhamu anazozichukua dhidi ya askari wanaokiuka maadili yao ya kazi. Akizungumzia suala hilo, Rais Magufuli amesema: “Endelea kuwa mkali ili kuimarisha nidhamu kwenye jeshi. Ukitaka kazi iende vizuri kufukuza lazima kuwepo, wapo watu wanaobambikiza kesi, wapo wanaohusika kwenye ujambazi, wapo wanaoonea raia hawa wachukuliwe hatua ingawa ni wachache sana.”Amesema. Kabla ya hapo jeshi hilo muhimu nchini humo lilikuwa likinyoshewa kidole cha lawama kutokana na baadhi ya askari wake wasio waaminifu kuhusika na matukio ya uhalifu, hususan ya kuwabambikizia kesi wananchi na matukio mengi kama hayo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇