Mwishoni mwa kikao cha nane cha kamati ya pamoja ya kibiashara ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan, nchi mbili zimetiliana saini makubaliano ya ushirikiano mjini Islamabad.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo ambayo yalitiwa saini na Reza Rahmani, Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Iran na Abdul Razak Dawood, Mshauri wa Waziri Mkuu wa Pakistan katika Masuala ya Viwanda na Biashara, pande mbili zitashirikiana katika uwanja wa ushirikiano wa kibiashara hususan katika maeneo ya pamoja ya mpakani, kustawisha shughuli za baharini na meli, pamoja na biashara nyingine. Kufanyika kikao hicho cha nane cha kamati ya pamoja ya kibiashara ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan mjini Islamabad, kunaakisi azma ya pande mbili ya kuboresha ushirikiano wao. Kuimarisha ushirikiano katika sekta ya kibiashara, kutumiwa nafasi zilizopo za nchi katika uga wa usafirishaji wa bidhaa za biashara, kuimarishwa miundombinu kwa ajili ya kurahisisha shughuli za usafirishaji na kuanzishwa maonyesho ya pamoja, ni masuala muhimu yaliyojadiliwa katika mazungumzo ya kikao cha nane cha kamati ya kibiashara ya Iran na Pakistan. Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Iran aliyewasili mjini Islamabad siku ya Alkhamisi, mbali na kushiriki katika kikao tajwa, pia alipata nafasi ya kukutana na Imran Khan, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Abdul Razak Dawood, Mshauri wa Waziri Mkuu katika Masuala ya Viwanda na Biashara, Zanbir Gilani, Mkuu wa Kamati ya Uwekezaji na Syed Ali Zaidi, Waziri wa Masuala ya Meli wa Pakistan, na kujadiliana nao kuhusiana na sekta za ushirikiano wa pande mbili.
Mazungumzo hayo na utilianaji saini wao, unabainisha uwepo wa irada ya pande mbili kwa ajili ya kuondoa vikwazo na kurahisisha mambo katika njia za kibiashara. Kwa kuzingatia upana wa mipaka yao na kuwa na tamaduni na historia inayofanana, nchi hizo zinaweza kuimarisha ushirikiano wao katika nyanja tofauti. Katika safari yake mwezi Aprili mwaka huu hapa nchini, Imran Khan Waziri Mkuu wa Pakistan alitiliana saini makubaliano muhimu yaliyofikiwa katika mazungumzo na jumbe za ngazi za juu za nchi mbili na hivyo kuufanya uhusiano wa Tehran na Islamabad kuingia katika hatua mpya. Katika mazungumzo ya waziri mkuu huyo wa Pakistan na ujumbe aliouongoza nchini hapa, Kiongozi Muadhamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, aliutaja uhusiano wa Iran na Pakistan kuwa uliokita mizizi moyoni na kusisitiza kuwa, mahusiano ya nchi mbili ni lazima yastawishwe na kuimarishwa licha ya kuwepo uadui unaofanywa dhidi ya nchi hizi. Hivi sasa hatua za mabadilishano kati ya Tehran na Islamabad katika uga huo, zinatoa ujumbe wa wazi kwamba uhusiano wa nchi mbili hizi unapita katika njia ya ustawi.
Aidha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan zikiwa nchi mbili waanzilishi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ECO na wanachama hai wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), zinatumia vyema nafasi zao kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano katika uga wa kiuchumi na biashara. Kuhusiana na suala hilo, Abdul-Muhammad Taher, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: "Islamabad inataka kuongeza ushirikiano wake wa kibiashara na majirani ili iweze kuinua uhusiano na nafasi yake ya kiuchumi, hasa ikizingatiwa kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha usalama na uchumi wa eneo na kuwa na nadharia chanya katika uwanja huo. Kwa mfano kuhusiana na bomba la kusafirisha gesi, Wapakistan wana matumaini makubwa ya kufanikishwa mradi huo. Mradi huo, hata hivyo haujafanikiwa kutokana na ukwamishaji mambo wa Marekani. Pamoja na hayo inaonekana kwamba katika safari hizi pande mbili zinaweza kupiga hatua nzuri katika uga wa kuimarisha biashara baina yao."
Katika uwanja huo Iran na Pakistan zimeazimia kuigeuza mipaka ya nchi mbili kuwa uwanja wa mabadilishano ya kibiashara yenye faida kwa ajili ya pande mbili sambamba na kuinua kiwango cha maisha ya wakazi wa maeneo hayo ya mpakani. Ushirikiano kama huo unaweza kuwa kiigizo chema cha kuigwa na majirani wengine. Harakati hiyo ya ushirikiano ya Iran inatekelezwa pia kuhusiana na nchi nyingine jirani zikiwemo za Afghanistan na Iraq. Umuhimu wa makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara yaliyotiwa saini kati ya Tehran na Islamabad, mbali na faida chanya za kiuchumi, unaweza pia kuimarisha usalama katika mipaka ya pamoja ya nchi mbili
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇