Waziri mkuu Ahmed aliwasili katika uwanja wa ndege wa Khartoum, na kuelekea moja kwa moja katika mazungumzo na majenerali wa Sudan ambao walimuondoa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir na kisha kuiongoza nchi. Baadaye, kiongozi huyo atafanya mazungumzo ya tofauti na viongozi wa waandamanaji. Ziara yake inakuja siku moja baada ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa kusitisha ushiriki wa Sudan kutokana na mgogoro huo.
Hayo yakijiri shirika la afya duniani WHO katika taarifa yake limesema linatiwa wasiwasi na matokeo ya vurugu za hivi karibuni katika upatikanaji wa huduma za afya kwa watu wa Sudan. Tarifa hiyo inasema hatua ya vikosi vya usalama kuvamia hospitali mjini Khartoum, ilisababisha huduma za dharura kusitishwa, wafanyakazi watano wa afya na wagonjwa kujeruhiwa pamoja na kuleta kitisho kwa wengine.
Waandamanaji wakiwa wamebeba picha ya kiongozi wa baraza la mpito la kijeshi
Vituo vya afya vilivyotengwa kwa ajili ya kuwahudumia waandamanji waliojeruhiwa vimechomwa moto, vifaa vya matibabu kuharibiwa na wahudumu wa afya kushambuliwa, kwa mujibu wa taarifa hiyo. Aidha shirika hilo limedai kuwa kumeripotiwa ubakaji wa wahudumu wa kike wa afya, na hivyo kutowa wito wa hatua kuchukuliwa na kwamba vitendo hivyo "havikubaliki na ni ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya haki za binadamu".
Uvamizi huo wa wanajeshi katika vituo vya afya unakuja baada ya vikosi vya usalama kuwashambulia waandamanaji wakati wa maandamano ya amani mjini Khartoum siku ya Jumatatu na kuwaua watu kadhaa huku mamia pia wakijeruhiwa.
Waandamanaji wanataka Baraza la kijeshi la mpito TMC kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia. Baraza hilo limekuwa madarakani tangu Bashir alipoondolewa mamlakani katika mapinduzi ya kijeshi yaliyofuatia miezi kadhaa ya maandamano dhidi ya serikali.
Siku ya Alhamis askari wa vikosi vya mgambo wanaotumiwa na idara ya usalama wa taifa RSF walivamia mji wa Khartoum na kuwalazimu wakaazi waliojawa na hofu kujificha ndani baada ya ukandamizaji uliofanywa dhidi ya waandamanaji wiki hii. Kwa mujibu wa mashuhuda askari hao walivamia Khartoum wakiwa katika magari ya kijeshi wakijihami kwa silaha nzito. Makundi ya haki za binadamu yanadai askari hao wanatoka kundi la wanamgambo la Janjaweed la jimboni Darfur.
dpa,afp
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇