LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 7, 2019

RAIS DK. MAGUFULI ATAJA CHANGAMOTO ZINAZOKWAMISHA KUKUA HARAKA KWA BIASHARA NCHINI

CCM Blog, Dar es Salaam
Rais Dk. John Magufuli amesema changamoto mbalimbali ambazo ni kikwazo cha kukua haraka kwa biashara hapa nchini kwa upande wa Serikali kuwa ni pamoja na wingi wa Taasisi za udhibiti zilizopo.

Taasisi hizo amezitaja kuwa ni kama TRA, OSHA, TBS, TFDA, Ofisi ya Mkemia Mkuuu, Tume ya Ushindani, EWURA, na SUMATRA ambazo amesema husababisha mwingiliano kimajukumu na kutoza tozo mbalimbali zinazofanana hivyo kudhoofisha ukuaji wa biashara.

Amesema, pia vitendo vya rushwa kwa baadhi ya watumishi wachache  wa Serikali wasio waadilifu 
hasa maeneo ya vizuizi barabarani, bandarini, na TRA, kuwa ni miongoni mwa changamoto inayorudisha nyuma jitihada za wafanyabiashara 

Rais amesema hayo, Ikulu jijini Dar es Salaam, akizungumza na Wafanyabiashara aliowaalika kutoka Wilaya zote nchini  ili kujadiliana nao kuhusu fursa na changamoto za biashara hapa nchini, mkutano ambao ulirushwa moja kwa moja kwenye vyombo mbalimbali vya habari.

Akitaja changamoto zinazosababishwa na Wafanyabiashara kukwamisha sekta ya biashara, Rais Magufuli amesema ni pamoja na ukwepaji kodi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara na vitendo vya utoaji rushwa.

Amesema kuna Kampuni 17, 446 zimekuwa zikikwepa kodi kwa njia ya mauzo hewa ya biashara za ndani na nje, manunuzi hewa kutoka Kampuni hewa ambapo ameagiza Kampuni hizo kuchunguzwa zaidi na zikithibitika kukwepa kodi zitalazimika kulipa kodi hiyo katika kipindi cha siku 30 kuanzia sasa.

''Baadhi yenu sio waaminifu mnakwepa kodi, mnatoa rushwa na wengine mmekuwa mkifanya kazi za udalali hasa kwenye biashara ya sukari, mafuta ya kula na korosho'' ameeleza Rais Magufuli

Rais alitaja changamoto nyingine kutoka kwa wafanyabiashara kuwa ni kuhujumu uchumi kwa kutokuwa wawazi katika mahesabu yao kwa kuwasilisha vielelezo tofauti vya taarifa ya fedha zinazopelekwa Benki na TRA.

Amewaonya wafanyabiashara wanaobadilisha matumizi ya viwanda yaliyokusudiwa awali wakati yakisajiliwa na kuanzisha biashara nyingine pasipo kufuata utaratibu.

Rais amezitaka Mamlaka husika katika Serikali kuweka mikakati thabiti ya kuwaendeleza wafanyabiashara wadogo na wakati kama ilivyofanyika kwa wafanyabiashara wakubwa.

''Wafanyabiashara wadogo na wakati ndiyo kitovu cha kukuza uchumi katika nchi, hivyo nashauri waendelezwe kama ambavyo tumeshaanza kwa kutoa vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo nchini'', alisisitiza Rais Magufuli.

Kwa upande mwingine, Rais amezionya taasisi za kifedha kutokana na kuwa na mitaji midogo huku zikiweka masharti magumu na kutoza riba kubwa ikiwemo kuendesha shughuli zake zaidi mijini kuliko vijijini.

''Serikali kupitia Benki Kuu imekuwa ikikopa fedha nyingi kwenye Taasisi za Kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia kwa ajili ya kutoa dhamana na kuwakopesha wajasiriamali wa hapa nchini, lakini sina hakika kama fedha hizo zinawafikia walengwa,'' amehoji Rais Magufuli.

Rais amewaonya mawakala wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) nje ya nchi wanaowasababishia hasara wafanyabiashara kwa kuidhinisha bidhaa ambazo zinagundulika kuwa hazina viwango zinapokaguliwa baada ya kuingizwa nchini.

Rais ameziagiza mamlaka husika kuangalia uwezekeno wa kuunganisha baadhi ya mifuko inayosimamia sekta ya biashara ili kuiimarisha na kupunguza gharama za uendeshaji huku akizitaka mamlaka zinazosimamia sekta ya biashara ikiwemo wizara, idara, wakala wa Serikali kuhakikisha changamoto hizo zinafanyiwa kazi mara moja ifikapo mwezi Julai mwaka huu, kwa kuzingatia mapendekezo yote yaliyomo katika kitabu cha mwongozo (Blue Print).

Katika kuhakikisha changamoto zilizopo zinatatuliwa, Rais ameitaja baadhi ya mikakati iliyowekwa na Serikali kuwa ni pamoja na kuandaa kitabu cha mwomgozo na kwamba mapendekezo mbalimbali yameanza kutekelezwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya biasha nchini.

Ameutaja mkakati mwingine kuwa ni Brela sasa kutumia utaratibu mpya wa kusajili biashara kwa njia ya mtandao, kufuta baadhi ya ada na tozo zilizokuwa zikitozwa na taasisi za OSHA na Zima moto kabla ya kuanzisha biashara.

Rais ametoa pongezi kwa wafanyabiashara a analog any a bias hara zao  kihalali ikiwa in pamoja na kufuata taratibu elekezi ikiwemo kulipa kodi kwa wakati.

Mkutano huo ni mwendelezo wa mikutano ambayo imekuwa ikifanywa na Rais kwa kuyahusisha makundi mbalimbali ikiwemo viongozi wa dini, wachimbaji wa madini, wazee na watendaji Serikalini lengo likiwa ni kujadiliana na kuweka mikakati itakayosaidia kukua kwa uchumi kwa maslahi ya Taifa.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages