Jeshi la Sudan limewatia mbaroni viongozi watatu wa upinzani muda mfupi baada ya viongozi hao kukutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.
Mohamed Esmat, mmoja wa viongozi wa Muungano wa Uhuru na Mabadiliko nchini Sudan ambaye amekuwa mstari wa mbele katika maandamano, alitiwa nguvuni na wanajeshi baada ya kukutana wa Waziri Mkuu wa Ethiopia siku ya Ijumaa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jana Jumamosi pia jeshi hilo lilimtia mbaroni Ismail Jalab, Katibu Mkuu wa Harakati ya Wananchi na Uhuru wa Sudan ikiwa ni baada ya kiongozi huyo pia kukutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia. Taarifa iliyotolewa na uongozi wa harakati hiyo ya wananchi imesema kuwa, askari hao walimkamata pia msemaji wake, Mubarak Ardwel.
Hayo yanajiri katika hali ambayo Jumatano iliyopita maafisa usalama wa Sudan walimtia mbaroni Yassir Imran, Naibu Kiongozi Mkuu wa Harakati ya Wananchi na Uhuru ya Sudan na kwenda naye kusikojulikana. Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed aliwasili mjini Khartoun, Sudan kwa ajili ya kufanya upatanishi kati ya wapinzani na askari wanaotawala nchi hiyo kwa sasa. Baada ya kukutana na Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Mpito Abdel Fattah Abdelrahman Burhan pamoja na baadhi ya viongozi wa upinzani alitoa pendekezo la kukabidhiwa madaraka kwa serikali ya kidemokrasia nchini humo. Mgogoro wa kisiasa nchini Sudan ulishika kasi baada ya jeshi la nchi hiyo kuwashambulia waandamanaji waliokuwa wamepiga kambi mbele ya makao makuu ya jeshi hilo ambapo kwa akali watu 108 waliuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇