Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) amewasilisha ombi la kutaka kufunguliwa upya faili la jinai za kivita za askari wa Marekani nchini Afghanistan kati ya mwaka 2003 na 2004.
Ombi hilo la Bensouda ni la kukata rufaa dhidi ya uamizi wa hivi karibuni wa majaji wa ICC wa kufunga faili hilo na kumuagiza Mwendesha Mashitaka Mkuu huyo wa mahakama hiyo iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi, asitishe azma yake ya kuanzisha uchunguzi wa jinai hizo za askari wa Marekani.
Tarehe 12 Aprili, ICC ilitangaza kuwa imeachana na suala la kufuatilia jinai za kivita zinazofanyika nchini Afghanistan kutokana na Marekani na madola mengine yanayoshiriki katika vita huko Afghanistan kukataa kushirikiana na mahakama hiyo ya kimataifa.
Taarifa ya mahakama hiyo ilisisitiza kuwa, hivi sasa mazingira hayaruhusu kufanyika uchunguzi wa kiadilifu nchini Afghanistan.
Hata hivyo mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu yameilaumu vikali Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kwa kufanya ubaguzi katika kazi zake. Shirika la Amnesty International limesema kuwa, kupinga ICC kufanyika uchunguzi kuhusu jinai za kivita za Marekani nchni Afghanistan kunaipotezea heshima na itibari mahakama hiyo ya kimataifa.
Kabla ya ICC kuchukua uamuzi huo, dola la kibeberu la Marekani lilikuwa limebatilisha viza ya Fatou Bensouda na kumpiga marufuku kuingia nchini humo ili kufuatilia kesi hizo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇