Kikosi cha Anga cha wapiganaji wa Jenerali Khalifa Haftar kimefanya shambulizi la anga lililolenga ghala la jeshi la Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa katika mji mkuu Tripoli na kuua watu tisa.
Msemaji wa Wizara ya Afya ya Libya, Fawzi Wanis amesema watu wote tisa waliouawa katika hujuma hiyo ya jana Jumamosi walikuwa raia.
Hata hivyo vikosi vya Haftar vinadai kuwa shambulizi lao lilipiga kwa ustadi ngome ya 'maadui' na kwamba hakuna raia aliyeuawa.
Hii ni katika hali ambayo, juzi Ijumaa, Umoja wa Mataifa ulisema mapigano mapya baina ya vikosi vya kamanda muasi wa Libya, Jenerali Khalifa Haftar na Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa katika mji mkuu Tripoli yamesababisha vifo vya raia 42, huku wengine zaidi ya 120 wakijeruhiwa.
Tarehe 4 Aprili mwaka huu Jenerali Khalifa Haftar siku chache baada ya kukutana na Mfalme Salman Bin Abdulaziz wa Saudi Arabia mjini Riyadh alitoa amri ya kushambuliwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Jenerali huyo muasi mbali na Saudi Arabia, anaungwa mkono pia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri, Ufaransa na Marekani.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO, mapigano hayo yamepelekea watu 653 kuuawa huku wengine zaidi ya 3,547 wakijeruhiwa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇