Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema zaidi ya watu laki tatu wameikimbia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, kutokana na mapigano ya kikabila.
Babar Baloch, msemaji wa UNHCR amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa, Wakongomani laki tatu wamekimbia mapigano ya kikabila katika mkoa wa Ituri, ulioko kaskazini mashariki mwa nchi. Mkoa huo ni moja ya maeneo yaliyoathiriwa na ugonjwa hatari wa Ebola nchini Kongo.
Hapo jana Jumatatu, maafisa wa serikali ya DRC walisema watu 161 wameuawa katika kipindi cha wiki moja iliyopita, kutokana na mapigano mapya baina ya jamii za wafugaji na wakulima katika mkoa huo.
Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, aghalabu ya wananchi wa DRC wanaoikimbia nchi wanatorokea katika nchi jirani ya Uganda, kupitia Ziwa Albert. Watu wawili waliaga dunia kutokana na ugonjwa huo siku chache zilizopita katika wilaya ya Kasese nchini Uganda, mpakani na DRC.
Makundi yenye silaha yamekuwa yakishambulia vituo vya matibabu mara kwa mara na kuwaua maafisa wa tiba wanaotoa huduma za kupambana na ugonjwa wa Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wizara ya Afya ya nchi hiyo imesema machafuko na hujuma dhidi ya makundi ya madaktari yanakwamisha zoezi la kupambana na ugonjwa wa Ebola na hivi sasa kesi mpya 1000 za ugonjwa huo hatari zimeripotiwa katika kipindi cha wiki 33 zilizopita.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇