Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu amesema kuwa Yemen imekumbwa na maafa mabaya zaidi ya kibinadamu kuwahi kushuhudiwa katika historia.
Mark Lowcock amesema kuwa zaidi ya nusu ya wananchi wa Yemen hivi sasa wanahitaji misaada ya kibinadamu. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa umoja huo unahitaji dola bilioni 4.2 ili kushughuligia mgogoro huo wa kibinadamu huko Yemen.
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) pia wiki iliyopita ulitahadharisha kuhusu maafa ya kibiandamu huko Yemen na kutangaza kuwa mama mmoja na wanawe sita hufariki dunia huko Yemen kila baada ya masaa mawili. Nao Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wenye mfungamano na Umoja wa Mataifa umesema katika ripoti yake ya karibuni kwamba hali ya kibinadamu huko Yemen ni ya kuhuzunisha sana na kutahadharisha juu ya kutokuweko usalama wa chakula kwa watu milioni 18 katika nchi hiyo iliyoathiriwa na vita.
Saudi Arabia huku ikiungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Marekani na nchi nyingine kadhaa waitifaki wake Machi 2015 iliivamia nchi maskini ya Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa baharini, ardhini na anga. Uvamizi huo wa kijeshi umeipelekea Yemen kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na dawa za matibabu mahospitalini.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇