Kamishna Mkuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa amewataka wanajeshi wa Sudan waache mara moja kuwakandamiza raia.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Michelle Bachelet alitoa mwito huo jana wakati wa kikao cha ufunguzi cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi na kuongeza kuwa, wanajeshi nchini Sudan wanapaswa kuacha kukandamiza maandamano ya wananchi na wawafungulie wananchi hao mawasiliano ya Intaneti.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, ofisi ya Kamisheni ya Haki za Binadamu ya umoja huo imepokea ripoti nyingi zinazoonesha kuwa zaidi ya raia 100 wa Sudan waliuawa tarehe 3 mwezi huu wa Juni mbele ya Wizara ya Ulinzi mjini Khartoum na mamia ya wananchi wengine hawajulikani walipo hadi hivi sasa.
Aidha Bachelet amelitaka jeshi la Sudan liruhusu wachunguzi wa kimataifa waingie nchini humo kufanya uchunguzi juu ya mauaji hayo ya umati. Hata hivyo majenerali wa kijeshi wa Sudan wamepinga mwito huo.
Sudan imekumbwa na maandamano makubwa ya wananchi tangu tarehe 19 Disemba 2018 yaliyopelekea kuanguka utawala wa karibu miaka 30 wa Omar al Bashir. Hivi sasa maandamano hayo ya wananchi yanaendelea ili kulishinikiza Baraza la Kijeshi la nchi hiyo kukabidhi madaraka kwa raia haraka iwezekanavyo.
Baraza hilo la mpito limehodhi madaraka ya Sudan tangu tarehe 11 Aprili mwaka huu. Wakati fulani baraza hilo lilifikia mapatano ya kukabidhi madaraka na wapinzani lakini lilivunja mapatano hayo na kuwaua kwa umati wananchi waliokuwa wamekusanyika mbele ya Wizara ya Ulinzi mjini Khartoum.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇