LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 25, 2019

TANZANIA YAITAKA CHINA KUZINGZTIA MANUFAA KWA PANDE MBILI KWA MIRADI INAYOWEKEZA NCHINI

Beijing, China
NCHI za Kiafrika zimeiomba China kuhakikisha kuwa ufadhili ama mikopo inayotoa kwa Nchi za Kiafrika inalenga katika miradi ya kikanda itakayoziunganisha na kuzinufaisha nchi hizo kiuchumi huku Tanzania ikiitaka China kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inayowekeza nchini iwe ya manufaa kwa pande zote mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi ameyasema hayo Beijing Nchini China katika mkutano wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) alipopata fursa ya kuzungumza katika mkutano huo na kuongeza kuwa endapo China itazisaidia kwa ufadhili ama kwa mikopo nafuu kuwekeza katika miradi hasa ya miundombinu itakayoziunganisha Nchi za kiafrika kwa kiasi kikubwa itazisaidia Nchi hizo kufanya biashara zenyewe kwa zenyewe  itaziwezesha kupiga hatua za kimaendeleo na kiuchumi na hivyo kujitegemea.

Ameongeza kuwa Mkutano huo wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) umekuwa ni wa manufaa kwa kuwa Nchi zenyewe za kiafrika zimepata fursa ya kutaja baadhi ya miradi ya kipaumbele kutokana na uitaji wa Nchi husika  huku akiitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji kwa kuwa Nchi nyingi za Kiafrika bado zina vyanzo vingi vya maji vinavyoweza kuzalisha umeme ambao utakuwa ni wa bei nafuu na kusaidia katika ujenzi wa viwanda.

Aidha katika mkutano huo wa siku mbili uliozikutanisha Nchi zipatazo 53 za Kiafrika na China zimeitaka China pia kuhakikisha inasaidia ama kufadhili katika kuinua uwezo wa kitaaluma utakaowawezesha vijana kwa Kiafrika kujiajiri na kupata wataalam wabobezi katika masuala mbalimbali kutokana na uwekezaji hasa wa viwanda na miundombinu utakaofanywa kwa pamoja na China na Nchi za Kiafrika.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo Prof. Kabudi amesema katika mkutano huo wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) Tanzania imesisitiza kuwa katika miradi ya uwekezaji,ya misaada ama ile ya mikopo nafuu inayoelekezwa Tanzania iwe ni ile yenye manufaa kwa pande zote mbili yaani win win situation kama anavyosisitiza Rais Dkt. John Magufuli.

Akisoma hotuba kwa niaba ya  Rais wa China Xi Jimping, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema kuwa China haitatoa misaada yenye masharti magumu kwa Nchi za Afrika, badala yake itaendeleza ushirikiano wake na Afrika katika kutekeleza miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa pande zote mbili.

Katika hotuba hiyo,serikali ya China imeahidi kuongeza umoja na ushirikiano kati yake na Afrika katika masuala ya kikanda na kimataifa ikiwa ni pamoja na kudumisha amani na usalama  ili kuleta maendeleo endelevu kwa watu na kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi.

Mkutano huo wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika limeazimia kwa pamoja kutekeleza miradi ya kipaumbele kulingana na uhitaji wa kila nchi kwa kufuata hatua nane zilizotangazwa katika mkutano wa wakuu wa nchi wa FOCAC uliofanyika mwezi September 2018 jijini Beijing.

Hatua hizo ni pamoja na program ya kuendeleza viwanda kupitia ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda,ujenzi wa miundombinu ikiwemo nishati,reli,barabara na bandari,sambamba na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vitakavyosaidia kuzalisha nguvu kazi ya viwandani.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages