Maafisa wa Saudi Arabia wamelazimika kusimamisha safari za ndege katika uwanja wa ndege wa Jizan wa kusini mwa nchi hiyo kufuatia shambulizi jipya la ndege isiyo na rubani (droni) ya jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen ambao wanajihami mbele ya uvamizi na mashambulizi ya kikatili ya Saudi Arabia na wavamizi wenzake.
Brigedia Yahya Saree, msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Yemen amesema kuwa, mashambulizi ya jana ya Jeshi la Anga la Yemen yalisambaratisha maeneo mengi muhimu ya Uwanja wa Ndege wa Jizan.
Mashambulizi ya jana yalikuwa ni utekelezaji wa kivitendo wa ahadi zilizotolewa na vikosi vya muqawama vya Yemen ambavyo viliahidi kushambulia maeneo muhimu ya wavamizi wa Yemen hasa Saudia na Imarati na vilisisitiza kuwa maeneo yote ya wavamizi wa nchi yao hayatobaki salama. Aidha mashambulizi hayo ni ushahidi mwingine kuwa vikosi vya muqawama vya Yemen vimeongeza nguvu zao katika kujibu mashambulizi ya wavamizi yanayoendelea kwa mwaka wa tano sasa dhidi ya wananchi maskini wa Yemen.
Hadi hivi sasa harakati ya Answarullah ya Yemen imeshafanya mashambulizi mengi ya makombora na ya kutumia ndege zisizo na rubani kwenye maeneo nyeti katika kona mbalimbali za Saudi Arabia na inaonesha wazi kuwa vikosi vya ulinzi vya Yemen vimepanua sana uwezo wao wa kijeshi.
Jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen miezi michache iliyopita zilitangaza kuwa, mwaka huu wa tano wa vita vya kujihami, utakuwa ni mwaka wa ushindi kwa wananchi wa Yemen.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇