Serikali imesema mabadiliko kwenye sekta ya sheria nchini hususani Ofisi ya Mwanasheria Mkuu yameanza kuleta tija baada ya kuongeza ufanisi na kuokoa fedha ambazo hapo awali zilikuwa zikitumika kuwalipa mawakili binafsi.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Augustine Mahiga alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), Saed Kuebenea lililokuwa likihoji juu ya kiasi cha fedha ambacho serikali imeokoa tangu maboresho kwenye sekta hiyo yaanze kutekelezwa, ambapo pamoja na mambo mengine yalianzisha Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo imepewa mamlaka ya kusimamia, kuendesha na kuratibu mashauri yote ya madai kwa niaba ya Serikali nchini.
Kwenye majibu yake Dkt. Mahiga alimueleza mbunge hyo kuwa kwenye Mwaka wa Fedha 2018/19 pekee Serikali imeweza kuokoa zadi ya shilingi bilioni tisa (9,018,957,011), ambazo kama sio maboresho kwenye sekta hiyo zingetumika kulipa makampuni binafsi ya uwakili.
Aidha, Dkt. Mahiga aliendelea kulieleza Bunge kuwa Serikali itaendelea kutumia Mawakili binafsi kwa kibali cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali pale itakapothibitika kuwa ni lazima kufanya hivyo. Alitoa mfano wa vigezo vinavyotumika kutumia mawakili binafsi ni shauri kufunguliwa kwenye mahakama ambazo sio za kimataifa na sheria za nchi husika haziruhusu uwakilishi wa mwanasheria kutoka nje ya nchi hiyo.
Kuhakikisha maslahi ya taifa yanalindwa Dkt. Mahiga ameliambia bunge kuwa uendeshaji wa mashauri hayo utendelea kuishirikisha Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwenye kila hatua ya mwenendo wake tofauti na hapo awali.
Kuhusu baadhi ya mashirika ya umma kuendelea kutumia mawakili binafsi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Adelardus Kilangi amelieleza Bunge kuwa mashirika hayo ni yale ambayo mashauri yake yalianza kabla ya maboresho kwenye sekta hiyo hayajaanza kutekelezwa na uendeshaji wa mashauri utatekelezwa kwa kushirikiana na Wakili Mkuu wa Serikali.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇