LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 13, 2019

MAZUNGUMZO YA WAZIRI MKUU

Shinzo Abe Waziri Mkuu wa Japan jana alasiri aliwaili hapa Tehran akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa nchi yake.
Siku ya kwanza ya ziara ya Waziri Mkuu wa Japan hapa nchini ilianza kwa yeye kufanya mazungumzo na Rais wa Iran. Waziri Mkuu wa Japan pia leo Alkhamisi amekutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei katika safari hii muhimu na ya kihistoria.
Wachambuzi wengi wa mambo wameitathmini ziara ya Waziri Mkuu wa Japan mjini Tehran katika fremu ya hamu ya Japan ya kukuza uhusiano wake na Iran. 
Shinzo Abe amesema mbele ya waandishi wa habari baada ya mazungumzo rasmi na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba: Anasisitiza hamu ya Tokyo ya kukuza uhusiano na Iran. Ziara hii ya Abe mjini Tehran pia ina umuhimu mkubwa kwa kuzingatia wasiwasi uliobainishwa na Japan kuhusu hali ya mvutano na mgogoro iliyojitokeza katika eneo la Asia magharibi. Kama alivyosema Waziri Mkuu wa Japan kwamba moja ya matarajio ya nchi hiyo ni kupunguza hali ya mivutano katika eneo la Asia magharibi na kwamba amefanya ziara nchini Iran kwa kulipa uzito suala hilo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema kuwa Waziri Mkuu wa Japan ana matarajio makubwa kuhusu masuala ya kieneo na kwamba: Iran inafurahishwa na msimamo wa Japan wa kuendelea kuyaunga mkono makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kutambua umuhimu wa makubaliano hayo kwa kanda hii na ulimwengu mzima kwa ujumla. Rais Hassan Rouhani amesema katika kikao cha pamoja cha jumbe za ngazi za juu za Iran na Japan kwamba,  nchi zote zina majukumu yanayoeleweka mkabala na makubaliano ya JCPOA na azimio nambari 2231 la Umoja wa Mataifa. Amesema anataraji kuwa Japan pia itatekeleza majukumu yake katika uwanja huo. 
Rais Hassan Rouhani akiwa na Waziri Mkuu  katika mkutano na vyombo vya habari
Pamoja na hayo yote, sehemu muhimu ya ziara hii ilihusu uhusiano wa nchi mbili. Hii ni kwa sababu safari hii ni ya kwanza kufanywa na Waziri Mkuu wa Japan nchini Iran baada ya kupita miaka 41. Safari ya Shinzo Abe ni ya pili kuwahi kufanywa na Waziri Mkuu wa Japan katika historia ya uhusiano wa nchi mbili hizi.  Salimi Namin mchambuzi wa masuala ya kisiasa na Mkurugenzi wa Ofisi ya Utafiti na Masuala ya Historia wa Iran anaamini kuwa: Japan kama yalivyo aghalabu ya madola mengine yenye uchumi uliostawi duniani kama China na India inaamini  kuwa mfumo wa kambi moja duniani umo katika hali ya kusambaratika na sasa inajaribu kuzidisha mahusiano kati yake na mataifa yenye nguvu kama Iran.  
Japan ni nchi ambayo imeonyesha katika siasa zake za nje kwamba inaamini misingi inayoongoza uhusiano wa kimataifa. Kwa msingi huo, inatazamiwa kwamba Abe, akiwa Waziri Mkuu wa Japan mwenye uzoefu mchungu kutokana na jinai zilizofanywa dhidi ya wananchi wa nchi hiyo kwa kushambuliwa kwa mabomu ya nyuklia na Marekani, atakuwa na uelewa mzuri zaidi kuhusu vitisho halisi katika eneo la Asia magharibi na ulimwenguni kwa ujumla na hivyo kufanya jitihada za kumaliza mvutano na hali ya wasiwasi iliyosababishwa Marekani na Israel dhidi ya amani na usalama eneo hilo. Ili kuweza kupata mafanikio katika uwanja huu inafaa kutambua kuwa, chanzo kikuu cha kuwepo mivutano katika kanda hii ni vita vya kiuchumi vilivyoanzishwa na Marekani dhidi ya Iran. Ni wazi kuwa hali ya mivutano itaendelea na kushtadi zaidi katika eneo hilo iwapo vita hivi havitahitimishwa.
Iran kwa upande wake inataka kuona amani na utulivu vinakuwepo katika sambamba na kuheshimiwa sheria za kimataifa. Kwa mtazamo huo, tunaweza kusema kuwa, ziara ya Waziri Mkuu wa Japan hapa Tehran kwa upande mmoja imelenga katika kukuza uhusiano na Iran na katika upande wa pili ni fursa ya kukurubisha mitazamo kati ya Tehran na Tokyo kuhusiana na masuala ya amani na usalama wa kanda hii. 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages