WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo
ya Makazi William Lukuvi ametangaza kupangwa kwa maeneo yote itakapopita reli
ya Mwendokasi (SGR) ili shughuli zitakazofanyika katika wilaya na vijiji
inapopita reli hiyo kwenda sambamba na shughuli za kiuchumi za mradi wa
reli hiyo.
Waziri Lukuvi alisema hayo tarehe 18
Mei 2019 katika vijiji vya Kwala na Soga vilivyopo Kibaha mkoa wa Pwani
alipozungumza na wananchi wa maeneo hayo kuwaelezea mpango wa Wizara yake
kupanga na kupima maeneo yote inapopita reli ya SGR ili kuendana na fursa za
kiuchumi za mradi wa reli hiyo.
" Wilaya na vijiji vyote reli ya
SGR itapita ardhi yao itapangwa na wale wananchi walio kando ya reli
itakapopita wasubiri wasiwe na wasiwasi ardhi ya maeneo yao itengenezewe
mpango na muongozo kuhusiana na maeneo hayo utatolewa" alisema Lukuvi.
Aidha, Lukuvi alisema wakati wa
kupanga maeneo hayo hakuna mwananchi yeyote atakayenyang'anywa eneo lake bali
maeneo hayo yatapangwa kimji na kuainishwa matumizi yake kama vile ujenzi wa
Viwanda na Mahoteli hivyo kuwataka wananchi wanaotaka kufanya uendelezaji mdogo
mdogo kusubiri mpango huo.
Alisema, lengo la serikali kupanga
maeneo hayo ni kutaka mpango mzima wa uendelezaji ukanda wa kiuchumi katika
maeneo hayo ufahamike kitaifa na kimataifa ili kuvutia wawekezaji watakaotaka
kuja kuwekeza na kubainisha kuwa fedha kwa ajili ya mpango huo zishatengwa.
Aliwatahadharisha wananchi wa vijiji
hivyo kutokubali kuanza kuuza maeneo yao kwa kuwa baada ya kupangwa kwa maeneo
hayo thamani ya ardhi itapanda na tayari baadhi ya watu wajanja kutoka nje ya
vijiji hivyo washaanza kutafuta maeneo kwa ajili ya fursa hiyo.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo
ya Makazi alisema, si vyema kila wilaya ikawa na mpango wake wa uendelezaji
maeneo itakapopita reli hiyo bali serikali inachotaka ni kuwa na mpango wa
kitaifa utakaotoa muongozo kwa wilaya zote kusisitiza kuwa ardhi katika maeneo
hayo itasimamiwa na wilaya husika.
" Tukiacha maeneo ya kandokando
ya reli bila kupanga na kupima kutafanyika vitu vya ajabu reli hii ina
faida kubwa hivyo lazima kupanga maeneo inakopita ili kwenda sambamba na
shughuli za kiuchumi za maeneo hayo" alisema Lukuvi.
Kwa mijibu wa Lukuvi, kuna timu
imeundwa kwa ajili ya Mpango wa Uendelezaji Ukanda wa kiuchumi katika eneo
inakopita reli ya SGR na timu hiyo inashirikisha wadau kutoka sekta
mbalimbali kama vile za Nishati, Uchukuzi, Reli na Mawasiliano lengo
likiwa kuwa na mpango utakaokidhi mahitaji ya uendelezaji ukanda kiuchumi
katika eneo linakopita reli ya SGR.
Mapema akiwa katika eneo inapojengwa
Bandari Kavu kijiji cha Kwala Kibaha vijijini, Mkuu wa wilaya ya Kibaha Asumpta
Mshana alimueleza Waziri Lukuvi kuwa wilaya yake ilipanga kuitumia fursa ya
reli hiyo pamoja na Bandari Kavu katika eneo la Kwala kwa ujenzi wa
Hoteli, Maduka makubwa (Malls) , Nyumba za kupangisha (Apartments) ili wale
wote watakaoitumia bandari hiyo kutoka maeneo tofauti waweze kupata malazi.
Akiwa katika Kwa Kijiji cha Soga
Waziri Lukuvi aliwaambia wananchi wa kijiji hicho kuwa, eneo lao lishapandishwa
hadhi na kuwa Mji hivyo ujenzi holela hautaruhusiwa na hati miliki za ardhi
zitakazotolewa eneo hilo ni miaka 99 na aliwataka wakazi wake
kuitumia fursa ya reli ya SGR kujiendeleza kiuchumi.
Mbunge wa Kibaha Vijijini
Hamoud Jumaa alimueleza Waziri Lukuvi kuwa zoezi la kuandaa mpango katika
maeneo hayo liende sambamba na uboreshaji miundo mbinu katika vijiji hivyo ili
kuwawezesha watu watakaoenda katika maeneo hayo kutokumbana na changamoto kama
vile barabara, maji na umeme.
This site truly has all the info I wanted concerning this subject and didn't know who to
ReplyDeleteask.