Akiwa anagubikwa na mlolongo wa tuhuma za rushwa, Netanyahu anawania muhula wa nne mfululizo pamoja na wa tano kwa ujumla, ambao utamfanya kuwa kiongozi wa muda mrefu zaidi nchini Israel, akimpita muasisi wa taifa hilo David Ben-Gurion. Anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mkuu wa zamani wa jeshi la Israel Benny Gantz, ambaye chama chake chenye kujitanabahisha kwa rangi za blue na nyeupe kilitajwa kukipita chama cha Netanyahu cha Likud kwenye kura ya maoni.
Nyota ya Netanyahu bado inawaka
Hata hivyo pamoja na matokeo hayo ya kura ya maoni kumweka mbele mkuu huyo wa majeshi wa zamani Netanyahu bado anaonekana kuwa na nafasi nzuri ya kuunda serikali ya mseto, pale ambapo vyama vidogo vya kizalendo vikimuunga mkono. Gantz akiwa na mke wake Revital, alipiga kura yake katika mji aliozaliwa wa Rosh Haayin, ulio katikati mwa Israel. Baada ya hatua yake hiyo alitoa wito kwa kila Muisrael kujitokeza kupiga kura akisema watapaswa kuwajibika kwa demokrasia yake. "Ninachoweza kusema, sisi sote tuheshimu demokrasia. Sote tunapaswa kuchukuwa wajibu wetu. Nenda kapige kura"
Akizungumza kabla ya kupiga kura yake Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema "Kabla sijapiga kura yangu, hii ni siku ya matumaini... hii ni siku ya matumaini, siku ya kuungana. Nikitazama macho ya kila mmoja unatambua kuna mawasilianio, najua tunaweza ungana. Na nina furaha ninaweza kuwahudumia raia wa Israel, kwa hivyo tunaweza kupanua wigo wa njia mpya, kuheshimu demokrasia, kutoa wito wa kuheshimiana na uchaguzi tulivu kwa pande zote. Na namtakiwa heri kila mmoja. Ahsanteni sana."
Vituo vya kupiga kura vilifunguliwa saa moja kamili Asubuhi na vinatarajiwa kufungwa saa 10 Alasiri. Takribani wapiga kura milioni 6.4 wanatarajiwa kushiriki zoezi hilo, kwenye vituo zaidi ya 10,000. Jumla ya vyama vya siasa 40 vinashiriki ingawa ni kumi tu miongoni mwa hivyo vinaweza kufanikiwa kuingia bungeni. Siku hii ya uchaguzi kwa Israel, ni siku ya mapumziko. Matokeo rasmi yanatarajiwa kuanza kutolewa Jumatano, ingawa inaweza kuchua muda kidogo kukamilika kwa matokeo kamili kutokana na hali ya mgawanyiko wa kisiasa ilivyo nchini humo.
Mwandishi: Sudi Mnette APE
Mhariri: Gakuba, Daniel
Mhariri: Gakuba, Daniel
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇