LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 11, 2019

RAIS DKT, SHEIN ALIPONGEZA SHIRIKISHO LA MICHEZO LA JUMUIYA YA MADOLA (IOC)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amelipongeza
Shirikisho la Michezo la Jumuiya ya Madola (IOC), kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha michezo mbali mbali nchini.

Dk. Shein ametowa pongezi hizo wakati alipokutana na Rais wa IOC Dame Louse Martin aliefika Ikulu na ujumbe wake kwa ajili ya mazungumzo.

Rais huyo wa IOC yupo Zanzibar kwa ajili ya kuhudhuria mkutano maalum wa Shirikisho la Michezo Jumuiya ya Madola (IOC), Kanda ya Afrika ulioanza jana katika hoteli Verde Mtoni mjini hapa.

Mkutano huo wa siku tatu unawashirikisha wajumbe kutoka nchi 19 za Afrika, ambapo pamoja na mambo mengine unatathmini maendeleo ya michezo katika kanda hiyo, ushindani wa kimichezo katika michuano ya Jumuiya ya Madola pamoja na ushiriki wa Kanda hiyo katika michuano ijayo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Birmigham nchini Uingereza, mwaka 2022.

Dk. Shein alisema kwa miaka kadhaa sasa IOC imekuwa ikiunga mkono kikamilifu juhudi za Serikali katika kuendeleza michezo mbalimbali nchini kupitia nyanja za kiufundi, mafunzo na rasilimali fedha.

Alisema hatua hiyo imeiwezesha Zanzibar kupata mafanikio makubwa ya michezo na hivyo kuleta
ushindani mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.

Naye, Rais wa IOC, Dame Louse Martin alimhakikishia Dk. Shein azma ya Shirikisho hilo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha michezo mbali mbali kupitia nyanja tofauti.

Alisema ameridhishwa sana na juhudi zinazochukuliwa na viongozi wa michezo nchini katika kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua kubwa za maendeleo kimichezo na kutajika duniani kote.

Katika ujumbe wake, Rais huyo wa IOC alifuatana na Makamu wa Rais wa IOC Kanda ya Afrika Miriam Moyo, Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Gulam Abdalla Rashid pamoja na Katibu Mkuu wa TOC Filbert Bayi.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages