LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 17, 2019

RAIS DK. MAGUFULI ATOA WIKI MOJA WIZARA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI NA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA KUKAMILISHA TARATIBU ZA UWEKEZAJI KWA KAMPUNI YA SUGAR INVESTMENT TRUST YA MAURITIUS

Rais Dk. John Magufuli akizungumza na Balozi wa Mauritius nchini Jean Pierre Jhumun pamoja na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk. Edwin Mhede, Maofisa wa Kituo cha uwekezaji na wa Ikulu baada ya kuonana na kufanya mazungumzo na balozi huyo Ikulu jijini Dar es Salaam, leo.

⇛Ikulu, Dar es Salaam
Rais Dk. John Magufuli ametoa wiki moja kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Viwanda na Biashara kukamilisha taratibu za uwekezaji kwa Kampuni Sugar Investment Trust (SIT) ya Mauritius ambayo imecheleweshwa kuwekeza katika uzalishaji wa sukari tangu mwaka juzi.

Rais ametoa maagizo hayo leo, Ikulu Jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuani hiyo Gansam Boodram aliyeongozana na Balozi wa Mauritius hapa nchini Mhe. Jean Pierre Jhumun.

Katika mazungumzo hayo Boodram alimweleza Rais kuwa yupo tayari kulima ekari 25,000 za mashamba ya miwa kwa ajili ya uzalishaji wa sukari na kwamba uwekezaji huo utawezesha kuzalishwa kwa tani 125,000 za sukari, ajira za kudumu 3,000 na ajira za muda 5,000 lakini amekwama kuendelea kutokana na kusubiri majibu ya Serikali kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusu upatikanaji wa eneo la uzalishaji wa miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari.

Rais Magufuli ameagiza ufanyike uchambuzi wa haraka katika maeneo ya Bonde la Mto Rufiji Mkoani Pwani, Eneo la shamba la Mkulazi Mkoani Morogoro na eneo la Kibondo Mkoani Kigoma ili mwekezaji huyo apatiwe na kuanza mara moja uwekezaji kwa kuwa nchi inahitaji kuongeza uzalishaji wa sukari utakaomaliza upungufu wa tani zaidi ya 100,000 ambazo kwa sasa zinaagizwa kutoka nje ya nchi.

Aidha, Rais amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Edward Mhede kufuatilia makubaliano ya ushirikiano katika uvuvi kati ya Tanzania na Mauritius ambayo hayajatiwa saini tangu mwaka 2017 licha ya wawekezaji wa Mauritius kuonesha nia ya kutaka kuwekeza katika uvuvi na viwanda vya samaki.

Balozi Jhumun amemueleza Rais kuwa Mauritius inao uzoefu mkubwa katika uvuvi na viwanda vya samaki na kwamba kwa kuitikia wito wake wa kuhamasisha wawekezaji kuja hapa nchini, amefanikiwa kupata kampuni zilizotayari kufanya uwekezaji huo baada ya makubaliano kati ya Tanzania na Mauritius kutiwa saini.

Rais amezionya taasisi za Serikali kikiwemo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kutoharakisha taratibu za kuwawezesha wawekezaji kuwekeza na amemhakikishia Balozi Jhumun kuwa atafuatilia kuhakikisha uwekezaji wa kampuni ya SIT unafanyika.

“Ndugu zangu watendaji wa Serikali badilikeni, achene kukwamisha wawekezaji, fanyeni maamuzi na kama yanawashinda toeni taarifa kwenye mamlaka za juu” amesisitiza Rais Magufuli.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages