Mahakama ya Juu nchini Uganda imeamua kuwa bunge la nchi hiyo lilifuata sheria wakati wa kuondoa kipengeie kilichozua mjadala mkubwa cha ukomo wa umri wa kugombea urais nchini humo, uamuzi ambao unampa nafasi Rais Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 74, kuwania tena urais mwaka 2021.
Wakiongozwa na Jaji Mkuu Bart Katureebe, Majaji wanne walitupilia mbali kesi hiyo ya upinzani huku Majaji watatu wakisema bunge halikufuata sheria wakati wa mabadiliko hayo. Uamuzi huo sasa unampa nafasi Rais Museveni ambaye amekuwa akiongoza Uganda tangu mwaka 1986 ya kuwania tena kiti hicho mwaka 2021 na kuendelea hadi mwaka 2026.
Mwanasheria Mkuu wa serikali Mwesigwa Rukutana amesema uamuzi huo wa Mahakama ni ushindi kwa wananchi wa Uganda.
Hata hivyo, wakili wa upinzani Erias Lukwago, amesema demokrasia ipo katika hali ngumu. Ameongeza kuwa, n masikitiko makubwa, lakini barani Afrika, ni miujiza kushinda kesi dhidi ya serikali iliyo madarakani.
Upinzani dhidi ya mabadiliko hayo ya sheria ulimuibua Mbunge kiijana Robert Kyagulanyi al-maaruufu Bobi Wine, ambaye kwa sasa amekuwa kama kinara wa upinzani na mwiba mkali dhidi ya serikali ya Museveni ndani na nje ya bunge la nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Wapinzani nchini Uganda wanalalamika na kuituhumu serikali ya Rais Yoweri Kaguta Museveni kwamba, imekuwa ikiendesha siasa za mkono wa chuma dhidi ya mrengo wa upinzani, hatua ambayo wanaitaja kuwa, inakandamiza na kubinya demokrasia katika nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇