Wanajeshi wa Marekani wakiwa chini ya ulinzi wa jeshi la SEPAH la Iran baada ya kuingia kwenye maji ya Iran kinyume cha sheria.
Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetangaza kuwa kikosi cha Marekani kilichopo katika eneo la Asia Magharibi (Centrecom) na askari wote walioko chini ya komandi hiyo ya kijeshi ya Marekani ni kundi la kigaidi.
Katika taarifa yake iliyoitoa leo, Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran limelaani hatua iliyo kinyume na sheria na hatari ya Marekani ya kuliweka jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Sepah katika orodha yake ya makundi ya kigaidi na kusema kuwa serikali ya Marekani ni muungaji mkono wa ugaidi hivyo wanajeshi wote wa Marekani waliopo katika eneo la Asia Magharibi na askari wote walioko chini ya komandi ya nchi hiyo, (Centrecom), ni kundi la kigaidi.
Taarifa ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran imeongeza kuwa, tofauti na walivyo Wamarekani ambao muda wote wamekuwa wakiunga mkono magenge yenye misimamo mikali na ya kigaidi katika eneo la Asia Magharibi, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH muda wote liko mstari wa mbele katika kupambana na magenge ya kigaidi kwenye eneo hili na muda wote wananchi wa nchi za eneo hili wamekuwa wakilipongeza jeshi hilo la kimapinduzi kwa msaada wake kwao katika kukabiliana na al Qaida, Daesh, Jabhatunnusra na magenge mengine ya kigaidi katika eneo hili.
Kabla ya hapo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikuwa amemwandikia barua Mkuu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran akimtaka awaingize wanajeshi wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi katika orodha ya Iran ya magenge ya kigaidi.
Katika kuendeleza uadui wake dhidi ya Iran, Marekani imetangaza kuwa imeliingiza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH katika orodha yake ya makundi ya kigaidi.
Leo pia msemaji wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Siasa za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) alikuwa amesema kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameionya Marekani isijaribu kuliingiza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH katika orodha yake ya makundi ya kigaidi, kwani Iran nayo itafanya hivyo hivyo kwa jeshi la Marekani.
Ali Najafi Khoshroudi aliliambia shirika la habari la Fars kwamba kikao kilichofanyika leo cha kamati hiyo kimehudhuriwa pia na Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kimejadili matukio ya siasa za nje na hatua zinazochukuliwa na chombo hicho cha kidiplomasia cha Iran.
Katika kikao hicho, Zarif alizungumzia tangazo la Marekani la kutaka kuliingiza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH katika orodha yake ya makundi ya kigaidi na kulaani nia hiyo ya Marekani akisisitiza kuwa, kitendo hicho kitakuwa na hatari nyingi na ijapokuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaki fujo lakini kama Marekani itachukua hatua hiyo, Iran nayo italipiza kisasi kwa kuchukua hatua kama hiyo dhidi ya jeshi la Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekosoa pia taarifa ya hivi karibu ya kundi la G7 na kusema kuwa taarifa hiyo inakwenda kinyume na vipengee vya mapatano ya nyuklia ya JCPOA.
Katika kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitza pia kuwa, safari za hivi karibuni za kutembeleana viongozi wa ngazi za juu wa Iran na Iraq ni tukio la kihistoria. Itakumbukwa kuwa baada ya Rais Hassan Rouhani kutembelea Iraq hivi karibuni, Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Adil Abdul Mahdi al Muntafiki, siku chache zilizopita alikuwepo hapa Tehran katika ziara rasmi ya kikazi nchini Iran.
Video hii hapa chini ni kumbukumbu ya tukio la kishujaa la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH la kuwatia mbaroni wanajeshi wa Marekani walipoingia bila ruhusa katika maji ya Iran Ghuba ya Uajemi mwezi Februari 2016.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇