Mripuko wa ugonjwa wa ebola umeua zaidi ya watu mia moja katika kipindi cha majuma matatu yaliyopita kwenye maeneo ya kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wizara ya Afya ya Kongo DR imetangaza kuwa, katika muda wa wiki tatu zilizopita, ugonjwa wa ebola umeua zaidi ya watu 100; na zaidi ya watu 700 wamefariki dunia tangu Agosti Mosi mwaka jana hadi sasa kutokana na ugonjwa huo hatari.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, kitovu cha ugonjwa huo ni eneo la kijiji kimoja kilichoko karibu na mji wa Beni.
Ripoti zaidi zinaeleza kuwa, maafisa wa Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hivi sasa wanawachunguza watu 295 wanaohofiwa kuambukizwa ugonjwa huo wa ebola.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa mripuko wa ugonjwa hatari wa ebola unasambaa kwa kasi nchini Kongo DR, ikiwa ni miezi minane sasa tangu ulipoanza kugunduliwa tena kwa mara ya pili.
Lakini mbali na ebola, ugonjwa wa surua pia umeshaua watu 800 tangu ulipoanza mwaka huu wa 2019 hadi sasa, kukiwepo na kesi 41,000 za watu wananaohofiwa kupatwa na ugonjwa huo.
Mripuko wa kipindupindu umeshuhudiwa pia nchini Kongo DR, ambapo tokea mwanzo wa mwaka huu hadi sasa watu wapatao elfu sita wameripotiwa kupatwa na ugonjwa huo, huku 140 kati yao wakiaga dunia.../
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇