Zimbabwe imeeleza kusikitishwa kwake na hatua ya Marekani ya kurefusha vikwazo dhidi ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika, inayokabiliwa na mgogoro wa kiuchumi.
Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Zimbabwe, James Manzou ameiambia Kamati ya Bunge la nchi hiyo kuwa, Marekani haikupaswa kurefusha vikwazo vyake dhidi ya nchi hiyo ambavyo vimeendelea kuwa na taathira hasi kwa uchumi unaoyumba wa Zimbabwe.
Hata hivyo amesema kuwa serikali ya Harare itaendelea kufanya mazungumzo na maafisa wa serikali ya Washington na nchi za Umoja wa Ulaya ili Zimbabwe iondolewa vikwazo vinavyoikabili.
Licha ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Rais Emmerson Mnangagwa kuiomba Marekani iifutie Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi, lakini Washington inasisitiza kuwa Marekani haitaondoa vikwazo ilivyoiwekea Zimbabwe hadi pale serikali mpya ya Rais Emmerson Mnangagwa itakapodhihirisha kuwa inabadili mielekeo yake.
Marekani inadai kuwa, sera za Rais Mnangagwa zingali ni 'tishio lisilo la kawaida' kwa sera za nje za Washington.
Mnangagwa ametoa wito wa kuondolewa vikwazo hivyo vya Marekani dhidi ya maafisa wa chama tawala Zanu-pf, maafisa wa ngazi ya juu wa jeshi na baadhi ya mashirika yanayomilikiwa na serikali vilivyowekwa wakati wa utawala wa Robert Mugabe kwa sababu ya kile ilichokitaja kuwa ni ukiukaji wa haki za binadamu na demokrasia.
No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇