LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 26, 2019

WAZIRI MKUU: WIZI WA MITIHANI UNALIVUNJIA TAIFA HESHIMA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa onyo kali kwa baadhi ya Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya wanaoshirikiana na waliamu kujihusisha na wizi, udanganyifu na uvujaji wa mitihani waache mara moja tabia hiyo na mwenendo huo kwa sababu unalivunjia heshima na hadhi Taifa.

“Kamati za Mitihani za Mikoa na Wilaya ziendelee kusimamia sheria, kanuni na taratibu bila ya woga, upendeleo na tusiyumbishwe na hatua za kinidhamu na kiutumishi kwa mujibu wa sheria.Hatua ziendelee kuchukuliwa dhidi ya wote wanaobainika kukiuka sheria, taratibu na miongozo inayotolewa”.

Waziri Mkuuametoa onyo hilo leo (Jumanne, Machi 26, 2019) wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Sita wa Umoja wa Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya(REDEOA), uliofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha Mipango jijini Dodoma. Kauli mbiu ya mkutano huo inasema “Elimu Bora Itatufikisha Katika Uchumi wa Kati Ifikapo 2025”

AmesemaBaraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) ni chombo ambacho kwa muda mrefu kimejijengea sifa kubwa sana nchini na barani Afrika, ambapo Serikali imewekeza kiasi kikubwa cha rasilimali ili kukifanya chombo hiko kuwa imara na cha kisasa. 

Waziri Mkuu amesema hali hiyo imezifanya nchi mbalimbali kuja nchini kujifunza masuala ya upimaji na uendeshaji wa mitihani. “Nimejulilishwa pia hivi sasa hapa nchini wapo Viongozi wa Mabaraza ya mitihani kutoka nchi za Afrika Mashariki”.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema suala la tatizo la nidhamu mbaya ya wanafunzi ni jukumu la walimu wote, hivyo wanatakiwa watekeleze majukumu yao ya kufundisha, kulea, kuwaongoza na kuwaendeleza wanafunzi kimwili, kiakili na kiroho kwa uadilifu na kuzingatia sheria. 

Waziri Mkuu amesema Serikali imesikitishwa sana na matukio ya hivi karibuni ya athari ya viboko kwa wanafunzi shuleni ikiwemo kuvunjwa mikono, kuachwa na makovu pamoja na tukio la kifo cha mwanafunzi Sperius Eradius wa shule ya msingi Kibeta Mkoani Kagera. 

“Ninatambua si kusudio la walimu kuwadhuru wanafunzi lakini tukubaliane kuwa kuna udhaifu katika utaratibu wa utoaji na usimamizi wa adhabu ya viboko shuleni. Maafisa Elimu kawakumbusheni walimu wote nchini wazingatie mwongozo wa kutoa adhabu shuleni chini ya kifungu cha 61 cha sheria ya Elimu sura 353 pamoja na kanuni zake”.

“Adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhamu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima. Na adhabu hii itatolewa kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi. Nina hakika tukisimamia utaratibu, matukio haya yaliyoanza kuonekana yatakoma”.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo amewapongeza maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya hao kwa sababu wanafanya kazi kubwa ambayo imechangia kupandisha ufaulu wa kidato cha sita na cha nne nchini. Amewasisitiza waendelee kufanya kazi kwa bidii.

Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewataka maafisa hao wawe wanatoa taarifa sahihi kuhusu idadi ya wanafunzi kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.

Awali, Mwenyekiti wa REDEOA, Germana Mung’aho amesema umoja wao unatekeleza majukumu yao ya kusimamia elimu kikamilifu nchini, lengo likiwa ni kumuunga mkono Rais Dkt. John Magufuli, ambaye anasisitiza watu wafanye kazi.

Amesema umoja huo una wanachama zaidi ya 400 na ulianzishwa ili kusimamia utoaji wa elimu nchini. Katika mkutano huo wanatarajia kujadiliana changamoto mbalimbali za sera ya elimu na namna ya kuzipatia ufumbuzi.

Kadhalika, Mwenyekiti huyo ameiomba Serikali iwapatie magari maafisa hao watakayoyatumia kwa ajili ya kufuatilia maendeleo ya elimu kwenye maeneo yao ya kazi, ambapo Waziri Mkuu amesema suala hilo linashughulikiwa.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages