Kiongozi wa wodi 4B MOI Bi Loema Nzugika akiwaeleza wataalamu kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania namna wanavyowahudumia wagonjwa wodini hapo
Kaimu Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi MOI Bw. Fidelis Minja (wa pili kushoto) akifafanua jambo wakati wa mafunzo maalum yaliyotolewa na wataalam kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga MOI leo. kuanzia kulia ni Muhasibu Baraza la Uuguzi na Ukunga Dinnah Daud, Afisa Muuguzi wa Baraza la Ukunga na Uuguzi Tanzania (TNMC) Bi. Happy Masenga na Afisa Muuguzi Baraza hilo Gustav Moyo. (PICHA ZOTE NA KHAMISI MUSSA)
NA KHAMISI MUSSA
WAUGUZI wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI)wamekumbushwa kuzingatia sheria na kanuni wakati wa utoaji huduma kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapo.
Akizungumza baada ya kutembelea hospitalini hapo, mwakilishi wa Msajili wa Baraza la wauguzi na wakunga Tanzania (TNMC), Happy Masenga alisema wauguzi wanatakiwa kuzingatia maadili ya taaluma yao.
Alisema kwa kuzingatia sheria ya Uuguzi ya mwaka 2010 walifika hospitalini hapo kujiridhisha kama huduma zinazotolewa zinakidhi viwango.
"Tumetembelea wodini kuangalia kama utoaji wa huduma unazingatia sheria na kanuni za uuguzi ambapo tumeridhishwa na hali tuliyoiona," alisema Happy.
Aidha alisema pia wameangalia utoaji mafunzo ya kujiendeleza kazini jambo ambalo amekiri kutekelezwa na MOI.
"Tunasimamia kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora na kwa ufasaha kulingana na taaluma," alisema Happy.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Uuguzi MOI, Fidelis Minja alisema pamoja na kuwapo kwa changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vitanda vyenye magurudumu lakini wauguzi hospitalini hapo wameendelea kutoa huduma bora.
"Pamoja na kukosa baadhi ya vifaa ikiwa ni pamoja na vitanda vyenye magurudumu tumeendelea kutoa huduma bora hasa kwa wagonjwa wa Ubongo wenye uhitaji wa vitanda hivyo," alisema Minja.
Alisema wauguzi wanatakiwa kutoa huduma wakiwa kwenye sare, ujuzi na uwezo wa kutoa huduma.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇