Rais Dk. John Magufuli
akiwasalimia wafanyakazi mbalimbali wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL)wakati
akitoka kukagua kazi ya upakaji rangi na uwekaji wa viti vipya katika ndege
aina ya Foker 50, leo.
Ikulu Dar es Salaam
Rais Dk. John Magufuli amefanya ziara ya ghafla kutembelea hanga la matengenezo ya ndege la Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kukagua marekebisho ya ndege ya Serikali aina ya Foker 50 ambayo inabadilishwa matumizi ili itumike kusafirisha abiria kama zinavyotumika ndege nyingine za ATCL.
Katika ziara hiyo Rais Magufuli ameshuhudia kazi ya ufungaji wa viti 48 vya abiria ukiwa umekamilika na mafundi wa kupaka rangi wakiwa wanakamilisha kuchora picha ya mnyama Twiga anayetumiwa kama nembo ya ndege za ATCL.
Rais Magufuli ameelezwa kuwa kazi ya marekebisho ya ndege hiyo imechukua muda wa siku 7 na mafundi wanakabidhi ndege leo, tayari kwa matumizi.
Tarehe 23 Desemba, 2018 wakati wa mapokezi ya ndege mpya ya Serikali aina ya Airbus A220-300 Jijini Dar es Salaam, Mhe. Rais Magufuli aliagiza ndege 2 za Serikali (Foker 50 na Foker 28) zilizokuwa zikitumiwa na viongozi zibadilishwe matumizi ikiwa ni pamoja na kupakwa rangi ya ATCL ili zitumiwe na Watanzania wote kwa kusafirisha abiria.
Hata hivyo mapema leo asubuhi akipokea taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mhe. Rais Magufuli ameeleza kusikitishwa kwake na kitendo cha viongozi na watendaji wa Serikali kutaka kupeleka ndege (Foker 50) Afrika Kusini ili ikabadilishwe rangi ambako ingetumia gharama kubwa ya kiasi cha zaidi ya shilingi Milioni 328 badala ya kazi hiyo kufanyika hapa hapa nchini.
Rais Magufuli amesema alilazimika kuingilia kati mchakato huo na kuagiza marekebisho hayo ikiwemo kupaka rangi za ATCL yafanyike hapa hapa Tanzania na zoezi hilo limefanikiwa kwa gharama ya shilingi Milioni 7 ikilinganishwa na shilingi Milioni 328 endapo ndege hiyo ingepelekwa Afrika Kusini.
Akiwa uwanjani hapo Rais Magufuli amemuagiza Mtendaji Mkuu wa ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi kuhakikisha fedha zote zilizoanza kutolewa kwa ajili ya kuipeleka ndege hiyo Afrika Kusini zikiwemo posho za marubani na wahudumu wa ndege, gharama za mafuta na malipo ya awali ya matengenezo zirudishwe.
Aidha, Rais Magufuli ameagiza mafundi 6 waliofanya kazi ya upakaji wa rangi ya ndege hiyo kwa makubaliano ya kulipwa shilingi Milioni 2 waongezwe fedha nyingine shilingi Milioni 10 kama motisha ya kuonesha moyo wa uzalendo, kufanya kazi kwa wakati na kuokoa fedha nyingi ambazo Serikali ingetoa kwa ajili ya kupeleka ndege Afrika Kusini.
Akitoa maelezo kwa Mhe. Rais Magufuli, Mhandisi Matindi amekiri kuwa endapo ndege hiyo ingepelekwa Afrika Kusini marekebisho yangetumia muda usiopungua siku 14 na gharama zingekuwa sio chini ya shilingi Milioni 328, na amemhakikishia Mhe. Rais Magufuli kuwa fedha zilizotolewa zimerejeshwa.
Mhandisi Matindi ameongeza kuwa baada ya kukamilika kwa matengenezo hayo ATCL inatarajia kuwa ndege hiyo itaanza mara moja kutoa huduma za usafiri wa anga katika kituo cha Mtwara na kufuatiwa na Iringa, Mpanda na baadaye Songea, Pemba na Tanga.
Rais Magufuli pia ametembelea hanga la ndege za Jeshi la Polisi na kushuhudia helkopta na ndege zilizopo, ambapo amelipongeza jeshi hilo kwa utunzaji mzuri wa ndege zake.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇