Rais
Dkt. John Magufuli amewahakikishia wanamichezo wote nchini ambao
wataliwakilisha vyema Taifa kuwa serikali itakuwa nao bega kwa bega ili
kuhakikisha wanaitangaza vyema nchi Tanzania.
Magufuli
ameyasema hayo leo Ikulu Dar es salaam wakati akizungumza na wanamichezo katika
hafla ya kuwapongeza kwa kufuzu (AFCON 2019), pia bondia Hassan Mwakinyo klishinda
pambano lake dhidi ya bondia Sergio Gonzalez wa Argentina lililofanyika Jijini Nairobi
nchini Kenya.
“Serikali
itaendelea kuunga mkono juhudi za wanamichezo wote kwa kuwa mafanikio yao
yanaliletea Taifa sifa na heshima na pia yanatangaza fursa mbalimbali ikiwemo
utalii, biashara na uwekezaji.” Amesema Magufuli.
Kuhusu matokeo
ya mchezo wa jana ulio zikutanisha Tanzania na Uganda Magufuli amewapongeza
wachezaji wa Taifa Stars, viongozi wa TFF, Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars na
Watanzania wote kwa kuungana pamoja kuishangilia timu yao katika mchezo wa jana
bila kujali tofauti zao za kidini, itikadi za kisiasa, makabila na kanda
wanazotoka.
“Kwa
kweli jana nilifurahi sana jinsi mlivyokuwa mnacheza na jinsi mlivyofunga
magoli, Watanzania wanataka furaha, sio kufungwafungwa kama mlivyofungwa kule
Lesotho, ile iliniuma sana hadi nilipanga kuwa sitaita tena timu kuja hapa
Ikulu, lakini sasa safi.” Alisema Magufuli na kuongeza kuwa
“Nataka
niwahakikishie Serikali ipo na nyinyi na ni matarajio yangu kuwa mtajiandaa
vizuri ili mkafanye vizuri katika michuano ya AFCON huko Misri, sasa vita
imeanza” amesema Magufuli.
Aidha Magufuli
amempongeza bondia Hassan Mwakinyo kwa ushindi alioupata hapo juzi baada ya
kumpiga kwa knockout bondia Sergio Gonzalez wa Argentina katika pambano lisilo
la ubingwa lilifanyika Jijini Nairobi nchini Kenya, pamoja na mapambano mengine
ambayo alishinda na amemtaka kuendelea kufanya vizuri katika mapambano mengine
ili kuipatia sifa Tanzania.
“Nafahamu
kuwa unazo changamoto nyingi ambazo hukusema hapa, lakini nakupongeza sana,
juzi umemtandika yule jamaa mpaka akakaa chini na huwa nakuona unavyofanya
mazoezi makali kwa kutumia matairi, wewe ni kijana safi sana” amesema Mhe. Rais
Magufuli
Hafla
ya kuwapongeza wanamichezo hao imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na
kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa Majaliwa, Viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Kamisheni
ya Ngumi Tanzania (TPBRC) na Kamati ya Ushindi ya Taifa Stars iliyoongozwa na
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.
Katika
hafla hiyo Magufuli amekubali maombi yaliyotolewa na Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya kusaidiwa maandalizi ya michuano ya
AFCON kwa vijana wa chini ya miaka 17 iliyopangwa kuanza tarehe 14 Aprili, 2019
hadi tarehe 28 Aprili, 2019 Jijini Dar es Salaam huku Tanzania ikiwakilishwa na
timu ya Serengeti Boys, ambapo amesema Serikali itatoa shilingi Bilioni 1
kusaidia maandalizi hayo.
Halikadhalika Magufuli ametoa zawadi ya kiwanja kimoja cha kujenga nyumba Jijini
Dodoma kwa kila mchezaji wa Taifa Stars, Bondia Hassan Mwakinyo, mchezaji
wa zamani na Nahodha wa Taifa Stars
Leodgar Tenga na mchezaji wa zamani na mfungaji wa bao lililoiwezesha
Tanzania kucheza robo fainali ya AFCON mwaka 1980 Peter Tino ambaye pia
amezawadiwa shilingi Milioni 5.
Kwa
upande wao wachezaji wa Taifa Stars ambao wameongozwa na Nahodha Msaidizi Himid
Mao na bondia Hassan Mwakinyo wamemshukuru Magufuli na Serikali kwa
ushirikiano mkubwa walioupata hadi kufikia mafanikio hayo na wamemuahidi
kuendelea kufanya vizuri katika michezo inayofuata.
Rais wa
TFF Wallace Karia na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Leodgar Tenga wamesema baada ya kufuzu kucheza fainali za AFCON sasa Taifa
Stars inaelekeza nguvu zake kujiandaa na michuano hiyo mikubwa Barani Afrika na
pia wameelezea matumaini makubwa ya Tanzania kufanya vizuri katika michuano ya
AFCON kwa vijana wa chini ya miaka 17 ambapo Tanzania itawakilishwa na timu ya
Serengeti Boys, michuano ya AFCON kwa wanawake ambapo Tanzania inawakilishwa na
Twiga Stars na kufanya vizuri kwa timu ya Taifa ya Soka chini ya miaka 20 (Ngorongoro
Heros) ambayo tarehe 31 Machi, 2019 itacheza na Eritrea Mjini Asmara.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇