Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema tatizo la saratani kwa Watanzania linaweza kupungua ama kuondokana nalo endapo kutakuwa na tabia ya kupima afya zetu mara kwa mara.
Makamu wa Rais ameyasema hayo leo kwenye uzinduzi wa jengo na mashine mpya za tiba ya mionzi LINAC ambazo ni za kisasa kabisa na kwa Afrika, Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kuwa nazo.
“tunaweza kujikinga kwa kufuata kanuni za afya zinavyotuelekeza kula chakula bora, kufanya mazoezi mara kwa mara, na kuepuka kunywa pombe kupita kiasi na kuepuka matumizi ya tumbaku”alisema Makamu wa Rais.
Mradi wa ununuzi na ufungaji wa mashine mpya za kisasa za tiba ya mionzi umegharamiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo shilingi bilioni 9.5 zimetumika.
Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha huduma za saratani hasa huduma za Kinga, Uchunguzi na Matibabu ya awali ikiwemo kuongeza vituo vya upimaji wa dalili za awali za Saratani ya mlango wa kizazi na matiti ambapo jumla ya vituo 650 vinatoa huduma hii kwa wakati.
Makamu wa Rais amewataka wananchi wote hasa wanawake kufika katika vituo ili kufanyiwa uchunguzi kwani zikigundulika dalili za awali mgonjwa atatibiwa na kupona.
Pia Makamu wa Rais amesisitiza wanaume waanze kuchukua mwamko wa kupima afya zao hasa kupima saratani ya tezi dume.
“Nashukuru Wizara kwa kuanzisha kampeni ya upimaji wa virusi vya ukimwi kwa wanaume, kwa kauli mbiu ya Furaha Yangu na ingefaa suala hili liende pia kwa upimaji wa Saratani ya Tezi Dume” alisisitiza Makamu wa Rais.
Mwisho, Makamu wa Rais ameupongeza mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kuingiza matibabu ya Saratani katika huduma ambazo wanagharimia“Ningependa kuwaagiza mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuhakikisha wanagharimia huduma hii ya tiba ya mionzi kwa LINAC.”
Wakati huohuo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema katika kipindi kifupi cha miaka mitatu sekta ya Afya imepata mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo chanjo kwa watoto zimefikia asilimia 98%, upatikanaji wa dawa muhimu ni asilimia 95%, vifaa na vifaa tiba, huduma za mama na mtoto ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya.
“Tumekusudia kuleta watalii wa matibabu”alisema Waziri Ummy
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇