Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, leo tarehe 29
Machi, 2019 imetoa Uamuzi wa kuifuta kesi Na. 22 ya Mwaka 2019 iliyofunguliwa
na Joshua Nassari aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki kutaka
arejeshewe Ubunge wake na imemuamuru alipe gharama za kesi hiyo.
Katika Shauri hilo Joshua Nassari alimshtaki Spika wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa madai
kuwa Spika ametoa uamuzi wa kumvua ubunge wake isivyo halali.
Uamuzi wa Mahakama wa kuifuta kesi hiyo umefikiwa baada ya
Serikali kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuweka Mapingamizi ya
Kisheria kutokana na kesi hiyo kukiuka misingi ya kisheria hivyo Wakili Mkuu
aliomba kesi hiyo itupiliwe mbali na Nassari alipe gharama za kesi.
Misingi iliyozingatiwa na Mahakama kutupilia mbali kesi hiyo
ni:
• Haikuwa sahihi kumshtaki Mheshimiwa Spika kwa kuwa
hakumvua Nassari ubunge wake bali aliijulisha Tume ya Uchaguzi kuwa nafasi ya
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki ipo wazi kutokana na kitendo cha Joshua
Nassari kushindwa kuhudhuria vikao vya Bunge vitatu mfululizo bila kuomba wala
kupewa ruhusa ya maandishi ya Spika.
• Hati ya Kiapo cha Joshua Nassari kilichowasilishwa
Mahakamani kilikuwa na dosari za kisheria kutokana na kiapo hicho kushuhudiwa
na Wakili aliyekuwa anamuwakilisha Mahakamani jambo ambalo ni kinyume na sheria
inayisimamia usimamizi wa viapo.
• Joshua Nassari
hakuwasilisha mahakamani uamuzi wowote anaoulalamikia kwamba umetolewa na
Mheshimiwa Spika bali aliambatisha Taarifa kwa Umma iliyotolewa na KItengo cha
Mawasiliano na uhusiano wa kimataifa - Bunge iliyofahamisha Umma kuwa
Mheshimiwa Spika amemtaarifu mwenyekiti wa Tume kuwa
“Ubunge wa Joshua
Nassari umekoma kutokana na kushindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge.”
Vile vile mahakama imeeleza kuwa, iwapo Joshua Nassari
anaamini kuwa Spika ametoa uamuzi dhidi yake basi anayo fursa ya kukata rufaa
dhidi ya uamuzi anaoulalamikia kwa mujibu wa kanuni ya 5(4) ya Kanuni za Kudumu
za Bunge, 2016 kwa kuwasilisha malalamiko hayo kwa Katibu wa Bunge ili
yafanyiwe kazi na Kamati ya Kanuni.
Baada ya kusikiliza Hoja za pande zote, Mahakama imeyakubali
Mapingamizi yote ya Mawakili wa Serikali na kuamua kutupilia mbali kesi
iliyofunguliwa na Joshua Nassari na kumtaka alipep gharama za kesi. Imetolewa
na: Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇