LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 24, 2019

UN YALAANI KUUAWA KWA ASKARI WAKE MALI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani shambulizi dhidi ya askari wa Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Mali (MINUSMA) katika eneo la Siby ambalo limesababisha vifo vya walinzi wa amani watatu kutoka Guinea na kuwajeruhi wengine.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa salamu za rambirambi kwa familia za wanajeshi waliouawa na kuwatakia nafuu ya haraka wale waliojeruhiwa.  Askari hao wa kulinda amani waliuawa Ijumaa katika hujuma iliyojiri katika eneo la Siby karibu na mji mkuu, Bamako.
Walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa na vikosi vya Ufaransa wako nchini Mali kupambana na makundi yenye silaha na ya kigaidi yenye uhusiano na kundi la Al-Qaeda, wanaotishia usalama kwenye eneo la Sahel.
Mwezi uliopita askari 12 wa MINUSMA, waliuliwa na wengine wasiopungua 25 kujeruhiwa wakati wakijaribu kuzima shambulio la watu wenye silaha karibu na kijiji kimoja kaskazini mwa Mali.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Antonio Guterres
Kikosi hicho cha MINUSMA kina askari 12,500 ambao walitumwa nchini Mali mwaka 2013 kwa ajili ya kuwadhaminia usalama raia, lakini vikosi hivyo havijakuwa na utendaji wa kuridhisha katika kurejesha utulivu huku vitisho vya ugaidi vikiendelea kuitatiza nchi hiyo. Hadi sasa askari wapatao 190 wa MINUSMA wameuawa wakiwa kazini.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages