Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wameitaka Ubelgiji iiombe radhi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na jinai ilizowafanyia Wakongomani katika kipindi cha ukoloni.
Katika ripoti yake ya awali iliyotolewa jana, Kundi la Wataalamu wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Watu Wenye Asili ya Afrika limesema kuwa, "Chimbuko la ukiukaji wa haki za binadamu hivi sasa, ni kutotambuliwa kina cha jinai na dhulma katika enzi za ukoloni."
Utawala wa Mfalme Leopold unakumbukwa kwa ukatili na jinai za kutisha katika enzi ambapo Kongo DR ilikuwa koloni la Ubelgiji, kati ya mwaka 1885 na 1908.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilijipatia uhuru na kujinasua kutoka kwenye makucha ya Mkoloni Mbelgiji mwaka 1960.
Ripoti ya mwisho ya Kundi la Wataalamu wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Watu Wenye Asili ya Afrika kuhusu jinai walizofanyiwa Wakongomani katika enzi za ukoloni inatazamiwa kutolewa mwezi Septemba mwaka huu.
Ubelgiji imesema inasubiri ripoti ya mwisho ya wataalamu hao wa UN, ili iitathmini na kutoa radimali yake.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇