LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 12, 2019

SIMBA SC YAIGONGA AL AHLY 1-0 NA KUFUFUA MATUMAINI YA ROBO FAINALI LIGI YA MABINGWA

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM

SIMBA SC imefufua matumaini ya kwenda Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Al Ahly kwenye mchezo wa Kundi D jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Pongezi kwa mfungaji wa bao pekee katika mchezo huo, mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere aliye katika msimu wake wa kwanza tu Simba SC tangu awasili kutoka Gor Mahia y Kenya.
Kagere alifunga bao hilo dakika ya 65 kwa shuti la mguu kulia akimalizia pasi ya kichwa ya Nahodha na mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, John Raphael Bocco kufuatia krosi ya beki Zana Coulibaly kutoka Burkina Faso.

Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi sita baada ya kucheza mechi nne ikipanda kwa nafasi moja hadi ya pili, nyuma ya Al Ahly wenye pointi saba na mbele ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yenye pointi nne na JS Saoura ya Algeria yenye pointi mbili.
Ikumbukwe JS Saoura wanaikaribisha AS Vita Saa 4:00 usiku wa leo Uwanja wa wa Agosti 20, 1955 mjini Bechar nchini Algeria.   
Simba SC watahamishia makali yao kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara wakimenyana na watani wao wa jadi, Yanga SC Jumamosi kabla ya kusafiri kuwafuata JS Saoura Machi 9 kabla ya kurejea nyumbani kumalizia na AS Vita Machi 16.
Timu mbili za juu zitaungana na washindi wengine wa makundi A, B na C kwenda Robo Fainali ya michuano hiyo. 
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Zana Coulibally, Asante Kwasi/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk39, Juuko Murshid, Serge Wawa, James Kotei/Muzamil Yassin dk90+2, Jonas Mkude, Clatous Chama, John Bocco/Hassan Dilunga dk82, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.
Al Ahly: Mohamed El Shenawy, Ayman Ashraf, Ali Maaloul, Yasser Ibrahim, Mohamed Hany, Amr Al Sulaya, Ramadan Sobhi, Karim Nedved/ Salah Mohsen dk84, Hussein El Shahat, Hamdi Fathi/ Nasser Maher dk70 na Oluwafemi Junior Ajayi.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages