Bunge la Seneti nchini Marekani linatazamiwa kujadili azimio lenye nia ya kuizuia Saudi Arabia kuunda silaha za nyuklia.
Rasimu ya azimio hilo iliwasilishwa jana na Maseneta wa chama cha Democrats Jeff Merkley na Ed Markey, pamoja na wa Republican Rand Paul. Hata hivyo haijabainika iwapo azimio hilo litaungwa mkono na aghalabu ya Maseneta, kutokana na uhusiano wa kimaslahi kati ya serikali ya Rais Donald Trump na utawala wa Aal-Saud.
Seneta Markley amesema, jambo la mwisho ambalo Marekani inaweza kufikia kufanya ni kuisaidia Saudia kuzalisha silaha za nyuklia, nchi ambayo ni haribifu katika jukwaa la kimataifa.
Mwezi Machi mwaka jana, Baraza la Mawaziri la Saudia lilipasisha sera kuu za kuanzisha miradi ya nyuklia ya nchi hiyo.
Hii ni katika hali ambayo, jarida la Foreign Policy la Marekani liliripoti kuwa, Saudi Arabia inataka kutengeneza silaha za nyuklia ikishirikiana na Marekani.
Jarida hilo lilisema Saudia sio nchi yenye utulivu wala inayopenda amani katika eneo la Mashariki ya Kati na kwa msingi huo haipasi kupewa mazingatio maalumu na serikali ya Marekani.
Mwaka jana, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia, Mohammed bin Salman aliiambia kanali ya televisheni ya CBS kuwa, Riyadh itaunda silaha za nyuklia iwapo Iran itafanya hivyo.
Hii ni licha ya kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ambayo ni mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa, haina nia wala haja ya kuunda silaha za nyuklia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇