LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 13, 2019

SAFARI YA KUSHTUKIZA YA KAIMU WAZIRI WA ULINZI WA MAREKANI NCHINI IRAQ

Baada ya baadhi ya maeneo ya Iraq kudhibitiwa na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) mnamo mwezi Juni 2014, Marekani iliimarisha uwepo wake ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu sambamba na kuweka askari wake katika kambi kadhaa za kijeshi katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.
Baada ya kutangazwa mpango wa kuondoka askari wa Marekani nchini Syria, Rais Donald Trump wa nchi hiyo alisema kwamba, askari wa Marekani watapelekwa Iraq. Wakati huo huo Trump alidai kwamba, kuna ulazima wa askari wa nchi hiyo kuwepo huko Iraq, kwa ajili ya kujiimarisha na kufuatilia harakati za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati. Pamoja na hayo, matamshi hayo ya Trump yamekabiliwa na radiamali kali ya Wairaqi. Hii ni kusema kuwa, Wairaqi wamepinga msimamo huo wa Trump wakisisitiza kuwa unalenga kukiuka haki ya kujitawala taifa hilo la Kiarabu. Baada ya rais huyo wa Marekani mwishoni mwa mwaka jana kutembelea ghafla kambi ya kijeshi ya askari wa Marekani nchini Iraq na kukutana na askari wa nchi yake, alionyesha kuwa ni mtu asiyeheshimu hata kidogo misingi ya kujitawala taifa hilo. Haidar Ali, mtaalamu wa masuala ya kisiasa nchini Iraq anasema, siasa zinazotekelezwa hivi sasa na Trump zinatofautiana na siasa za hapo kabla za Washington, kwa kuwa siasa hizo zinatekelezwa kwa njia ya moja kwa moja huku zikiitambua Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa adui nambari moja na kutaka Iraq iwe uwanja wa kukabiliana na Iran.


Trump alipotembelea ghafla kambi ya askari wa Marekani nchini Iraq 

Ni kwa kuzingatia tofauti za wazi zilizopo kati ya Washington na Baghdad, na katika juhudi za kujaribu kutatua tofauti hizo na kuwavutia viongozi wa ngazi ya juu wa Iraq kwa ajili ya kuridhia kuendelea kuwepo askari wa Marekani nchini humo, ndipo Patrick M. Shanahan, Kaimu Waziri wa Ulinzi wa Marekani akafanya safari ya kushtukiza nchini Iraq asubuhi ya Jumanne iliyopita. Katika safari hiyo ambayo ilikuwa haijatangazwa na Pentagon, Shanahan alikutana na Adil Abdul-Mahdi, Waziri Mkuu wa Iraq na makamanda wa jeshi la Marekani. Kwa mujibu wa ripoti ya vyombo vya habari vya Iraq, safari ya kaimu waziri huyo wa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, ilifanyika kwa lengo la kuchunguza kadhia ya kuondolewa askari wa nchi hiyo kutoka Syria na vile vile mustakbali wa uwepo wa askari hao nchini Iraq. Hii ni katika hali ambayo Marekani inadai kwamba, uwepo wa askari wake nchini Iraq, una nafasi athirifu katika mapambano yake na kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) na kuwafurusha magaidi wa kundi hilo kutoka maeneo ya nchi hiyo ya Kiarabu. Hata hivyo inajisahau kwamba, yenyewe ndiye muhusika mkuu katika kuanzishwa na kupanuliwa harakati za kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) kuanzia mwaka 2011. Hata katika kampeni za uraisi wa Marekani mwaka 2016, Trump aliitaja bayana serikali ya mtangulizi wake, Barack Obama kuwa muhusika mkuu wa kuanzishwa genge hilo hatari la kigaidi. Hata hivyo katika matamshi yake mapya amedai kwamba hivi karibuni atatangaza habari ya kutokomezwa kikamilifu kwa kundi la Daesh nchini Iraq na Syria.


Askari wa Marekani nchini Syria

Akitoa hotuba katika kikao cha viongozi wa muungano wa kimataifa unaoitwa, eti ulio dhidi ya Daesh (ISIS) huko mjini Washington, tarehe 6 ya mwezi huu, Trump aliweka bayana kwamba, kuna uwezekano akatangaza ndani ya kipindi cha wiki moja ijayo kwamba muungano huo wa Kimarekani umefanikiwa kulitokomeza kikamilifu kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh nchini Iraq na Syria. Iwapo jambo hilo litafikiwa, basi kazi muhimu inayofuatiliwa kwa sasa na Wizara ya Ulinzi ya Marekani ni kuwaondoa askari wa Marekani kutoka Syria ambayo kwa mujibu wa Pentagon, itatekelezwa hivi karibuni. Kwa mujibu wa Jenerali Joseph Votel, Mkuu wa Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM), kuondoka askari wa nchi hiyo kutoka Syria kutaanza ndani ya kipindi cha wiki chache zijazo. Hivi sasa Marekani ina karibu askari 2000 nchini Syria ambao akthari yao ni wa kutekeleza operesheni maalumu na ambao wanashirikiana pia na wapiganaji wa kundi la Kiarabu linalojiita 'Syrian Democratic Forces.' Inaonekana kwamba serikali ya Marekani na kwa kisingizio cha kupambana na kundi la Daesh (ISIS) itawahamisha askari wake kutoka Syria na kuwapeleka Iraq kama ambavyo pia imejiandaa kuendeleza wakati wowote ule uingiliaji wake wa kijeshi nchini Syria. Safari ya Patrick M. Shanahan, Kaimu Waziri wa Ulinzi ya Marekani nchini Iraq pia imefanyika kwa ajili ya kuweka wazi namna ya uwekaji wa askari hao na jinsi watakavyochangia katika kile kinachoitwa na Washington operesheni za kijeshi za kupambana na kundi la Daesh. Bila kusahau kwamba suala la uwepo wa Iran nchini Iraq na malalamiko ya Washington juu ya suala hilo ni nukta nyingine iliyotazamiwa kujadiliwa katika mazungumzo ya Shanahan na viongozi wa ngazi ya juu wa Iraq.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages