Ubakaji wa kikatili aliofanyiwa msichana wa miaka mitano na mjomba wake umetoa mtikisiko nchini Sierra kwa kampeni ya kupambana na ovu hilo na kumpa msukumo rais wa nchi hiyo Julius Maada Bio kuutangza ukatili wa kingono kuwa ni hatari ya kitaifa inayohitaji hatua za haraka.
Binti huyo wa miaka mitano ambaye jina lake limehifadhiwa kwa ajili ya usalama wake, amepooza kuanzia kiunoni hadi miguuni tangu jamaa yake huyo mwenye umri wa miaka 28 alipombaka kimabavu mwaka mmoja uliopita na kumvunja uti wa mgongo. Akizungumza na vyombo vya habari katika kliniki moja mjini Freetown, kando ya mjukuu wake aliyekuwa ameketi kwenye kiti cha magurudumu, bibi wa mtoto huyo amevieleza vyombo vya habari kuwa huenda msichana huyo asiweze kutembea tena na kusisitiza kuwa, aliyemharibia maisha yake anastahiki kumalizia maisha yake jela.
"Ninatangaza ubakaji na ukatili wa kingono kuwa ni hatari ya kitaifa", alisema Rais Bio hapo jana wakati akihutubia hadhara ya wananchi Ikulu mjini Freetown kufuatia kilio kikubwa cha ongezeko la vitendo vya ubakaji na ukatili wa kingono nchini humo.
Kiongozi huyo amesema, watu watakapotikana na hatia za kuwabaka watoto wadogo watapewa adhabu ya kifungo cha maisha jela.
Ripoti zinaeleza kuwa theluthi moja ya waathirika wa vitendo hivyo ni watoto wadogo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Polisi ya Sierra Leone, idadi ya kesi za ukatili wa kingono na unyanyasaji wa kijinsia iliongezeka maradufu mwaka uliopita wa 2018 kwa kuripotiwa matukio zaidi ya 8,500 kulinganisha na 4,750 ya mwaka 2017 katika nchi hiyo yenye watu wapatao milioni saba na nusu. Hata hivyo wanaharakati, akiwemo mke wa rais Bi Fatima Bio wanasema, idadi halisi ya matukio hayo ni kubwa zaidi kwa sababu kesi nyingi za vitendo hivyo huwa haziripotiwi.
Imeelezwa kuwa wengi kati ya waathirika wa ubakaji huambukizwa maradhi ya uasherati vikiwemo virusi vya HIV na mamia ya wengine hupata ujauzito.
Uamuzi wa Rais Julius Maada Bio wa kutangaza ubakaji kuwa tatizo hatari kwa taifa unaonekana kuwa ni hatua yenye muelekeo mzuri, lakini wanaharakati wanasema, uchukuaji hatua zaidi unahitajika hasa ikizingatiwa kuwa wahusika wengi wa ovu hilo hukwepa mkono wa sheria.
Katika kesi kubwa ya ubakaji iliyoripotiwa mwaka jana, mahakama moja ya mjini Freetown ilimhukumu kifungo cha mwaka mmoja tu jela mwanamme mwenye umri wa miaka 56 aliyepatikana na hatia ya kumbaka binti wa miaka sita.../
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇