Mamlaka ya hali ya hewa nchini (TMA) imetoa mwelekeo na hali ya mvua za masika kwa mwezi Machi hadi Mei mwaka huu kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua na kutoa angalizo kwa Wananchi kufuatilia mirejesho inayotolewa na mamlaka hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Dkt. Agnes Kijazi amesema kuwa mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka na kueleza kuwa maeneo ya Nyanda za juu Kaskazini mashariki yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Dkt. Kijazi amesema kuwa mvua za masika ni mahususi katika maeneo ya Nyanda za juu kaskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini na visiwa vya Unguja na Pemba, Ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini wa Mkoa wa Kigoma na sehemu kubwa ya maeneo hayo yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani katika msimu wa masika kwa mwaka 2019 na katika baadhi ya maeneo ya nyanda za juu Kaskazini mashariki hasa katika Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro uwezekano wa wa kunyesha kwa mvua za juu ya wastani ni mkubwa.
Akifafanua hali ya kunyesha kwa mvua hizo Dkt.Kijazi amesema kuwa kwa maeneo ya ukanda wa ziwa Viktoria kwa Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita,Simiyu na Shinyanga Dkt. Kijazi amesema kuwa mvua kwa maeneo hayo zinatarajiwa kuanza kunyesha wiki ya nne ya mwezi Februari katika Mkoa wa Kagera na kusambaa katika mikoa ya Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga katika wiki ya pili ya mwezi Machi. Na mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi na upungufu wa mvua unatarajiwa katika maeneo machache Mkoa wa Kagera na Wilaya ya Kibondo.
Amesema kuwa katika ukanda wa Pwani ya Kaskazini ikihusisha Mikoa ya Dar es salaam, Tanga Pwani, Visiwa vya unguja na Pemba pamoja na Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro ambapo mvua katika maeneo hayo zinatarajiwa kuanza kunyesha wiki ya kwanza ya mwezi Machi katika Mkoa wa Dar es salaam, Pwani na Visiwa vya Unguja na Pemba na kusambaa katika Mkoa wa Tanga na Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro katika Wiki ya kwanza ya mwezi Machi na mvua hizo zinatarajiwa kuwa hadi juu ya wastani katika maneo mengi na upungufu wa mvua unatarajiwa kutokea katika Mkoa wa Morogoro.
Kwa upande wa nyanda za juu Kaskazini Mashariki ikiwa ni kwa Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara mvua kwa maeneo haya zinatarajiwa kuwa za juu za wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro na kwa maeneo ya Mashariki mwa mkoa wa Kilimanjaro (same) na maneo mengi ya Mkoa wa Manyara yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇