Huku Mapinduzi ya Kiislamu yakiwa yanaadhimisha miaka 40 ya umri wake, kombora jipya erevu la balistiki la ardhi kwa ardhi linaloitwa Dezful limezinduliwa.
Katika sherehe za uzinduzi wa kombora hilo jipya hapo jana Alkhamisi, kiwanda cha kutengeneza makombora ya balistiki cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, pia kilizinduliwa. Akizungumza katika sherehe za uzinduzi huo, Muhammad Ali Jaffari, Kamanda Mkuu wa SEPAH alisema kuwa kuzinduliwa kwa kiwanda cha kutengeneza makombora hayo ya balistiki katika kina kirefu chini ya ardhi ni jibu la moja kwa moja kwa matamshi ya kipuuzi na yasiyo na maana ya Wamagharibi ambao wanadhani kwamba kwa kuiwekea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikwazo na kuitisha wanaweza kuibana na kuizui kufikia malengo yake makuu. Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, SEPAH, amesema kwamba kwa kuadhimisha miaka 40 y umri wake, Mapinduzi ya Kiislamu yanatangaza wazi kufikia uwezo wake kamili wa kiulinzi na kuongeza kuwa uwezo wa kiulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ni wa kumfanya adui asithubutu kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi yake na kwamba ni katika msingi wa kulinda usalama wa kitaifa ambao hauwezi kufanyiwa mapatano ya aina yoyote ile. Kabla ya uzinduzi wa kombora hilo la balistiki la Dezful, siku ya Jumamosi kombora jingine la masafa marefu la Cruise linalojulikana kama 'Huwaizeh' lilizinduliwa.
Kombora hilo ambalo limeundwa kutokana na teknolojia ya kisasa kabisa na ambalo limetengenezwa na wataalamu wa humu humu nchini lina uwezo wa kusafiri umbali wa kilomita 1,350 na linatumika kulenga shabaha zisizohamishika. Kuandaliwa haraka, kupaa kwa masafa ya chini angani, umakini katika kupaa na ulengaji shabaha pamoja na uharibifu mkubwa wa shabaha inayolengwa ni miongoni mwa sifa za kombora hilo la Huwaizeh. Kombora la Khorramshah, ni kombora jingine jipya la balistiki la Iran ambalo lina uwezo mkubwa wa kusababisha uharibifu na ambalo linaoongozwa kwa mitambo maalumu hadi linapofikia shabaha iliyokusudiwa. Bila shaka uwezo wa kiulinszi wa makombora ya Iran umefikia kilele cha ukamilifu katika kipindi cha miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu na jambo hilo bila shaka linathibitisha wazi kuwepo elimu, teknolojia na maarifa ya juu katika sekta ya ulinzi ya Iran. Mafanikio hayo yote yamefikiwa katika hali ambayo, tokea ushindi wa Mapinduziya Kiislamu, Iran imekuwa ikikabiliwa na vikwazo vya aina mbalimbali kutoka nchi za Magharibi na hasa Marekani. Bila shaka jambo hilo linaoonyesha wazi kwamba nara ya "Sisi Tunaweza" imethibiti wazi katika sekta ya ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ni wazi kwamba katika mazingira hayo, vikwazo na kuongezwa mashinikizo dhidi ya Iran hakutaweza kuizuia kufikia mafanikio na ustawi zaidi katika sekta hiyo.
Uundaji makombora na kudhihirishwa teknolojia na elimu tofauti katika sekta ya ulinzi ya Iran kumeifanya sekta hiyo isiweza tena kuathiriwa na vikwazo na bila shaka kuzinduliwa kwa kiwanda cha chini ya ardhi cha kutengeneza makombora ya balistiki cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPEH, ni ujumbe tosha kwa Ulaya na Marekani kwamba kamwe Iran haitaomba idhini kwa mtu yoyote katika juhudi zake za kuimarisha usalama wake wa kitaifa. Akizungumzia uwezo wa makombora ya Iran hapo siku ya Jumamosi, Brigedia Generali Hussein Salami, Naibu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kwamba kufikia sasa Iran haijawahi kukabiliwa na tatizo lolote la kiteknolojia katika jitihada zake za kuimarisha uwezo wa makombora yake, na hasa kuhusiana na suala la umakini wa kulenga shabaha, fueli na teknolojia ya kisasa ya makombora, bomu linalobebwa na kombora, uharibifu wa kombora na uwezo wa kombora kukwepa rada. Uwezo wa kiulinzi wa Iran kupitia makombora mbalimbali ya kibalistiki unafuatiliwa katika fremu ya mfumo wa ulinzi wa kitaifa. Hatua za majeshi ya Iran katika kipindi cha miaka 40 iliyopita zimekuwa zikichukuliwa katika mtazamo wa kujilinda na kumzuia adui kuanzisha mashambulizi ya kichokozi. Hatua hizo hizo bado zinafuatiliwa kwa makini na hasa katika mazingira ya hivi sasa ambapo adui amezidisha vitisho vyake na wala Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaomba idhini kutoka kwa nchi yoyote ile kuhusiana na suala la kujidhaminia usalama wake kama ilivyoainishwa katika sheria za kimataifa. Nguvu ya makombora na kiulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina ujumbe wa amani na urafiki kwa marafiki wa Mapinduzi ya Kiislamu, nchi za eneo na majirani wa Iran.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇