Waziri wa zamani wa Vita wa utawala haramu wa Israel ametoa wito wa kuanzishwa tena siasa za mauaji dhidi ya viongozi na wanamapambano wa Kipalestina huko katika Ukanda wa Gaza.
Avigdor Lieberman amesema kuwa, kuna uwezekano wa kutokea mapigano na vita vingine katika Ukanda wa Gaza na kuongeza kuwa, haipaswi kukaa na kusubiri kuona yakitokea mauaji dhidi ya wanajeshi wa Israel.
Waziri wa zamani wa Vita wa utawala haramu wa Israel alijiuzulu cheo hicho Novemba 14 mwaka jana baada ya kuanza duru mpya ya mizozo na mashambulio katika Ukanda wa Gaza na majibu ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS dhidi ya mashambulio ya wanajeshi wa utawala huo ghasibu.
Avigdor Lieberman, alikuwa akipinga usitishaji vita huko Gaza hata hivyo kwa mujibu wa Wapalestina, Baraza la Mawaziri la Israel lililazimika kukubali usitishaji vita katika eneo hilo baada ya wanamapambano wa Kipalestina kuvurumisha makombora katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Hivi karibuni Avigdor Lieberman alinukuliwa akisema kuwa, katika vita vya siku mbili kati ya Israel na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS, Tel Aviv ililazimika kutangaza usitishaji vita siku mbili tu baada ya harakati hiyo kuvurumisha zaidi ya makombora na maroketi 500 upande wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
"Uvurumishaji wa makombora na maroketi zaidi ya 500 kutoka Ghaza dhidi ya vitongoji vya Israel, ni kufeli kukubwa kwa baraza la mawaziri la Netanyahu." Amesema Avigdor Lieberman.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇