LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 12, 2019

HASIRA ZA TRUMP KWA USHIRIKI MKUBWA WA WANANCHI WA IRAN KATIKA MAADHIMISHO YA USHINDI WA MAPINDUZI YA KIISLAMU

Rais Donald Trump wa Marekani amekuwa akiishambulia Iran kwa maneno makali iwe ni katika kipindi cha kampeni za uchaguzi mwaka 2016 au baada ya kuingia katika Ikulu ya White House Januari mwaka 2017 na hivyo kuendeleza mkondo wa kutakka kuudhoofisha na kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unaotawala hapa nchini.
Donald Trump aliingia katika vita vya kiuchumi na Iran baada ya kutoa tangazo la kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Hatua ya Trump ya kurejesha vikwazo vya nyuklia dhidi ya Iran ililenga kueneza umasikini na machafuko nchini Iran. Katika upande wa kieneo pia, serikali ya Trump kupitia stratejia ya usalama wa taifa ya mwaka 2017, imefanya juhudi kubwa za kuanzisha miungano ya kikanda kwa shabaha ya kuikwamisha Iran na wakati huo huo kufanya hima ya kubadilisha siasa na hatua za Tehran katika eneo la Mashariki ya Kati.
Pamoja na hayo yote, lakini hatua za serikali ya Trump za kuikwamisha na kuishinda Jamhuri ya Kiislamu zimeshindwa na kugonga mwamba. Hasa mahudhurio makubwa na ambayo hayajawahi kushuhudiwa ya wananchi wa Iran katika maandamano ya jana Bahman 22 ya maadhimisho ya ushindi ya Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yamemfanya Trump achanganyikiwe.
Maandamano ya maadhimisho ya miaka 40 ya ushindi wa mapinduzi ya Kiislamu ya Iran
Akionyesha kukasirishwa kwake na mahudhurio hayo makubwa, Rais Trump aliweka ujumbe wa lugha ya Kifarsi na Kiingereza katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter. Katika ujumbe wake wa hapo jana usiku kwa mara nyingine tena Trump alitoa madai yasiyo na msingi na yenye kuchekesha kwa kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba, eti inaunga mkono ugaidi na kwamba, kwa muda mrefu sasa Wairani wamekuwa wakiishi kwa tabu na wanastahiki mustakabali bora.
Trump anajifanya kwamba, ana uchungu na wananchi wa Iran ilihali tangu aingie madarakani ameiwekea vikwazo vikali na vyenye wigo mpana Iran akifanya juhudi za kuipigisha magoti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na hivyo kuifanya ibadilishe misimamo na mitazamo yake. Hivyo ni kichekesho kwa mtu kama Trump kudai kwamba, anaguswa na hali ya kiuchumi ya wananchi wa Iran.
Licha ya njama zote za Marekani, lakini katika kipindi chote cha miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wananchi wa Iran wamethibitisha kwamba, hakuna wakati ambao wako tayari kuipa mgongo Jamhuri ya Kiislamu kwa kuathiriwa na domokaya, propaganda na mashinikizo ya serikali ya Washington, na hivyo waache mamlaka yao ya kujitawala na kufuata matakwa ya kimabavu ya dola la kibeberu la Marekani.
John  Bolton, mshauri wa usalama wa taifa wa Ikulu ya Marekani, White House
John  Bolton, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa serikali ya Marekani ambaye amekuwa akidhihirisha waziwazi uadui wake mkali dhidi ya taifa la Iran, naye alitoa matamshi sawa na ya bosi wake.
Baada ya mamilioni ya wananchi kushiriki jana katika maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Botlon alitoa ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter akikariri madai dhidi ya Iran na kuandika: Baada ya miaka 40, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshindwa kutekeleza majukumu yake ya kulinda na kutetea haki za raia wake.
Ukweli wa mambo ni kuwa, Marekani inajidanganya kwa kudhani kwamba, kwa kutumia propaganda chafu na kuishinikiza Iran kiuchumi itafanikiwa kuifanya isalimu amri na hivyo kutekeleza matakwa yake. Kupitia vikwazo vya kiuchumi, serikali ya Trump inafanya kila iwezalo ili kuyafanya maisha ya wananchi wa Iran yawe magumu na ya kuumiza na kwa muktadha huo kama inavyodai, eti iandae mazingira ya kutokea vurugu na machafuko hapa nchini.
Sera hizi za Marekani kimsingi ni uingiliaji wa wazi wa masuala ya ndani ya Iran, hatua ambayo ni kinyume kabisa na sheria za kimataifa. Vilevile hatua hiyo inakinzana kabisa na kanuni za kimataifa na hata hati ya Umoja wa Mataifa. Hapana shaka kuwa, mwenendo huu wa Trump dhidi ya Iran unazidi kuthibitisha kwamba, Rais huyo wa Marekani hajui chochote kuhusiana na Wairani. Tajiriba ya miaka 40 iliyopita inaonyesha kuwa, kadiri mashinikizo kutoka nje dhidi ya Iran yanapoongezeka, basi ndivyo mshikamano wa ndani unapoimarika.
Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran 
Katika majibu yake kwa ujumbe uliokuwa umejaa hasira na vinyongo wa Rais Donald Trump wa Marekani, Dakta Muhammad Javad Zarif, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Baada ya miaka 40 ya machaguo yasiyo sahihi, umewadia wakati sasa kwa "Donald Trump" kutazama upya siasa zilizoshindwa na kufeli za Marekani mkabala wa Iran.
Licha ya madai ya Trump ambaye amefanya kadiri awezavyo kuishinikiza na kuitenga Iran, lakini walimwengu hivi sasa wameng'amua vyema kwamba, njama za serikali ya Trump za kutaka kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu chimbuko lake ni chuki na adawa za Marekani dhidi ya Iran hasa kutokana na kusimama kidete taifa hili mbele ya matakwa ya kibeberu na yanayoingilia masuala ya ndani ya Iran na Mashariki ya Kati. Kimsingi sera za Marekani za kutaka kuuangusha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu zimepelekea kuongezeka mshikamano wa kitaifa baina ya Wairani na wakati huo huo kuimarika moyo wao wa kuchukia ubeberu na Uistikbari.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages