Februari 7, 2019, Akiwa katika ziara ya Kata kwa kata ya uhuishaji wa hai wa Chama na ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya Mwaka 2015 – 2020 Mkoa wa Arusha, Wilaya ya Arusha Mjini katika Kata za Engutoto, Lemara, Muriet, Terrat, Olasiti na Osunyai Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi amesema CCM inawaonya viongozi wake wote wa Serikali za Mitaa wasiowajibika kusoma mapato na matumizi na chama kimeahidi kutowarudisha katika uchaguzi wa serikali za mitaa Mwaka huu 2019.
Akifafanua suala hilo Ndg. Polepole amesema kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa viongozi wote wasiowajibika, wasio soma mapato na matumizi kwa mujibu wa sheria, wenye tabia za kupokea au kutoa rushwa Chama hakitawavumilia na hawatapewa fursa ya kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2019.
*"Tunaposimamisha wagombea wa CCM kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa wa 2019 tunahitaji watu mwenye tabia nzuri, waaminifu, wanyenyekevu, wachapakazi, wapole lakini wakali kwenye mambo ya hovyo na wanaokubalika kwa watu”* amesisitiza Ndg. Polepole
Aidha akiwa katika ziara hiyo Ndg. Polepole amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa jengo la cha Wagonjwa wa Nje (OPD) la hospitali ya Wilaya ya Arusha Jiji lililopo katika Kata Engutoto, Ujenzi wa barabara kuu ya mchepuko (kilometa 42. 4 kwa kiwango cha lami) yenye madaraja 7, ujenzi wa maabara katika shule ya Sekondari Terrati katika Kata ya Muriet, Ujenzi wa madarasa manne katika shule ya msingi muriet Darajani na ujenzi wa barabara ya Sombetini FFU yenye urefu wa kilometa 2.1 kwa kiwango cha lami.
Huu ni muendelezo wa Ziara za ujenzi wa Chama na ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Mwaka 2015 – 2020.
Imetolewa na,
*IDARA YA ITIKADI NA UENEZI*
*CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM*
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇