Benki Kuu (BoT) imezindua Mfumo wa Malipo ya Papo kwa Papo Tanzania (TIPS) wenye lengo la kurahisha kufanya malipo mbalimbali ya miamala ya fedha kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa uhakika na salama zaidi.
Uzinduzi huo umefanyika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini Dar es Salaam ambapo viongozi wa ngazi mbalimbali kutoka taasisi za fedha na serikalini wamehudhuria huku Naibu Gavana wa BoT Dk.Benard Kibese akitumia uzinduzi huo kufafanua umuhimu wa mfumo huo kwa kina.
Akizungumza zaidi wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Mifumo ya Malipo wa Taifa ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bernard Dadi amesema Mfumo wa Malipo ya Papo kwa Papo Tanzania(Tanzania Instant Payment System) utamuwezesha utumaji wa fedha toka taasisi moja kwenda nyingine kufanya malipo bila kutumia fedha za kampuni nyingine.
"Kwa hiyo tutakuwa mfumo pale BOT ambao sasa mteja wa kampuni moja kwa mfano Vodacom anaweza kutuma fedha kwenda kwenye benki yoyote ile bila gharama. Kwa mfumo huu tutakuwa na majina sehemu moja kwa hiyo ukituma fedha ule muamala ambao umetumwa hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi wa jipa kwani kupitia mfumo huu utachukua jina kamili na kutuma kwa mteja tena kwa usalama kwani jina na fedha zitakuwa zimehakikiwa.
"Mfumo huu tunatarajia utajengwa ndani ya miezi 18 kupitia watalaamu wetu wa ndani ya BoT pamoja na wataalam wa taasisi nyingine za fedha na baada ya hapo sasa tutakwenda ndani zaidi kwa kuhakikisha tunamhudumia mteja wa kijijini kwa haraka na uhakika zaidi.Hivyo kupitia mfumo huu tunaamini sasa huduma za kufanya malipo ya fedha uko salama zaidi,"amesema.
Amefafanua sababu za kuiita mfumo huo ni Instant maana yake ni kwamba ndani ya sekunde moja hadi mbili fedha itakuwa imemfikia mteja tena ikiwa kamili bila kukosewa wakati kabla ya mfumo huo wapo ambao wamekuwa wakilalamika fedha kwenda kwa watu ambao si walengwa kutokana na kukosewa kwa jina au namba iliyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇