Waziri wa Ulinzi wa Venezuela, Vladimir Padrino LĂłpez amesema kuwa, Marekani na washirika wa White House ndio wanatekeleza mapinduzi ya kijeshi na vita vya kiuchumi dhidi ya nchi hiyo.
Padrino López ameyasema hayo wakati akilaani uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini na kusisitiza kuwa Rais Nicolás Maduro ndiye rais halali wa Venezuela. Ameongeza kwamba, wapinzani nchini humo wako katika kutekeleza mapinduzi hayo dhidi ya rais huyo. Wakati huo huo Eliot Engel, mkuu wa kamati ya masuala ya kigeni wa bunge la wawakilishi nchini Marekani ametoa taarifa inayounga mkono ghasia na machafuko nchini Venezuela na kusisitiza kwamba Marekani iko pamoja na waandamanaji huko Venezuela.
Jumanne iliyopita Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na bila kuzingatia chaguo la wananchi wa Venezuela waliomchagua Nicolás Maduro, aliingilia wazi wazi masuala ya ndani ya nchi hiyo na kumtaka rais huyo aondoke madarakani na kumpisha Juan Guaido, anayeungwa mkono na nchi za Magharibi. Katika hali ambayo ghasia zinazidi kuongezeka nchini Venezuela, serikali ya Mexico kwa mara nyingine imetaka kufanyika mazungumzo nchini humo na kufikiwa utatuzi kwa mzozo kwa njia ya amani. Juan Guaido alijitangaza kuwa rais wa muda wa Venezuela Jumatano iliyopita suala ambalo limelaaniwa vikali na serikali ya Caracas.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇