Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu ya Umoja wa Mataifa ametilia mkazo udharura wa kushirikiana na Iran katika uwanja wa kupambana na dawa hizo na kusema Jamhuri ya Kiislamu inashika nafasi ya kwanza duniani katika kupambana na dawa za kulevya.
Yuri Fedotov ameyasema hayo katika mazungumzo yake na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Iran Naser Seraj huko Vienna, Austiria. Amesema kuwa ushirikiano wa Iran na Umoja wa Mataifa katika kupambana na dawa za kulevya upo katika kiwango kizuri na kuongeza kuwa, Umoja wa Mataifa unawajibika kusaidia na kuunga mkono kazi na shughuli zinazofanywa na Iran katika uwanja wa kupambana na dawa za kulevya kwa kutayarisha mazingira yanayofaa na vyanzo vya fedha.
Kwa upande wake Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Iran ameashiria tatizo kubwa la dawa za kulevya dunia na kazi zilizofanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupambana na janga hilo ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za mali na hali zilizotumiwa katika uwanja huo na amezikosoa nchi mbalimbali na jumuiya za kimataifa kutokana na kutoshiriki ipasavyo katika vita hiyo. Naser Seraj ameutaka Umoja wa Mataifa kuimarisha vyanzo vya fedha na kupanua zaidi ushirikiano katika uwanja huo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kupambana na magendo ya dawa za kulevya duniani imepoteza zaidi ya askari elfu nne waliouawa katika vita vya kupambana na magenge ya magendo ya dawa za kulevya. Askari wengine elfu 12 wamejeruhiwa katika uwanja huo.
Umoja wa Mataifa umeitaja Iran kuwa ni mbeba bendera ya mapambano dhidi ya mihadarati duniani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇